Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania kivutio kikubwa cha utalii Afrika 2022

81cf8d0227972f348ac7707e33a91d40.PNG Tanzania kivutio kikubwa cha utalii Afrika 2022

Tue, 8 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Sekta ya utalii nchini ina mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa nchi. Kabla ya mlipuko wa janga la Covid-19 kuikumba dunia, sekta hiyo ilikuwa ikichangia takribani asilimia 17.2 ya pato la taifa, asilimia 25 ya mauzo ya nje na asilimia 60 ya mapato yote yatokanayo na biashara za huduma nchini.

Pia sekta hiyo imekuwa ikichangia katika uchumi wa nchi zaidi ya Sh trilioni 6.0 na kuzalisha ajira takribani milioni 1.5.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro anaeleza hayo wakati akielezea maendeleo ya sekta hiyo nchini kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2021. Dk Ndumbaro anasema Covid-19 imeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii nchini ikiwa ni pamoja na masoko makuu ya utalii kama ambavyo imebainishwa katika taarifa mbalimbali za Shirika la Utalii Duniani (UNWTO).

Kwa upande wa Tanzania, waziri huyo anasema idadi ya watalii waliotembelea nchini ilipungua kutoka 1,527,230 mwaka 2019 hadi 620,867 mwaka 2020 sawa na upungufu wa asilimia 59.3. Anasema pia mapato yatokanayo na utalii yalipungua kutoka Dola za Marekani bilioni 2.6 mwaka 2019 hadi Dola za Marekani bilioni 0.715 mwaka 2020 sawa na upungufu wa asilimia 72.5.

“Madhara ya Covid-19 hayakuathiri Tanzania pekee, bali pia nchi za ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla. “Mfano taarifa za taasisi ya Baraza la Usafiri na Utalii Duniani (WTTC), zinaonesha kuwa nchi tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki zilipokea jumla ya watalii wa kimataifa milioni 2.16 mwaka 2020 ikilinganishwa na milioni 7.05 kwa mwaka 2019,” anasema.

Anasema mapato yatokanayo na shughuli za utalii yalishuka kutoka Dola za Marekani bilioni 6.1 mwaka 2019 hadi Dola za Marekani bilioni 1.9 mwaka 2020. “Pia inakadiriwa kuwa ajira zilipungua kutoka milioni 4.1 hadi milioni 2.2 mwaka 2020 ambayo ni anguko la asilimia 48,” anasema.

Ndumbaro anakiri kuwa pamoja na athari hizo, mwaka jana yalianza kuonekana matumaini mapya kwa sekta ya utalii. Hivyo idadi ya watalii duniani inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia nne ikilinganishwa na idada ya watalii kwa mwaka juzi. “Katika Bara la Afrika, idadi ya watalii inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 12 ikilinganishwa na idadi ya watalii wa mwaka juzi,” anasema.

Kwa upande wa Tanzania, idadi ya watalii iliongezeka kwa asilimia 48.6 kutoka watalii 620,867 mwaka juzi hadi watalii 922,692 mwaka jana. Anasema mapato yatokanayo na watalii wa kimataifa yanakadiriwa kuongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 1,254.4 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 76. “Ongezeko hili linashabihiana na ongezeko la mapato ya nchi jirani ya Kenya ambapo mapato yaliongezeka kwa asilimia 65 kutokana na ongezeko la asilimia 57 la idadi ya watalii,” anasema.

Ndumbaro anasema kuimarika kwa utalii nchini kumetokana na mwelekeo na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuanzisha na kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa kukabiliana na janga la Covid-19 nchini. Anasema mpango huo wa kitaifa umeleta taswira mpya kiutalii ambapo Tanzania imekuwa eneo salama zaidi kutembelewa na watalii. “Utalii pia umekuwa ni miongoni mwa sekta za kipaumbele kwa wafanyakazi wake kupatiwa chanjo hiyo. Vile vile serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeanzisha vituo viwili vya kuchukulia sampuli kwa ajili ya kupima Covid-19 katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na pia kuweka maabara maalumu ya kupima ugonjwa huo katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro,” anasema.

Anasema pia kumekuwa na jitihada maalumu za Rais Samia katika kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia programu maalumu ya Royal Tour. Kupitia programu hiyo mtandao maarufu wa habari nchini Marekani wa theGrio umetambua juhudi hizo za Samia katika kuiongoza vyema sekta ya utalii nchini na kuifanya Tanzania kuwa kivutio cha kwanza cha utalii Afrika mwaka 2022.

“Programu hii kwa ujumla imeanza kuleta matunda kwa kuvutia watalii na wawekezaji kuja nchini. Mathalani, wakala wa utalii zaidi ya 30 kutoka nchi zenye masoko ya utalii yakiwemo Marekani, Ufaransa na Lithuania wamehamasika kutembelea nchini ili kujifunza na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii kwa lengo la kuvitangaza katika nchi zao,” anasema. “Aidha, wizara inakamilisha makubaliano na wakala mkubwa wa kutangaza utalii katika soko la Marekani ikiwa ni pamoja na kufungua ofisi ya kutangaza utalii nchini humo,” anasema.

Anasema pamoja na ongezeko la idadi ya watalii wa kimataifa, katika kipindi Nyumbu katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. cha mwaka 2021, idadi ya watalii wa ndani waliotembelea maeneo ya hifadhi pia iliongezeka kutoka 562,549 mwaka 2020 hadi watalii 788,933 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 40.2. Pia mapato yatokanayo na utalii wa ndani katika maeneo yaliyohifadhiwa yaliongezeka kutoka Sh bilioni 9.7 mwaka juzi hadi Sh bilioni 12.4 mwaka jana sawa na ongezeko la asilimia 27.8.

Anasema serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Covid-19. Katika mpango huo Wizara ya Maliasili na Utalii imetengewa Sh bilioni 90.2 sawa na asilimia 6.9 ya fedha yote kwa ajili ya utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali.

Fedha hizo anaeleza kuwa zitawezesha taasisi za wizara hiyo kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuimarisha masoko na utangazaji utalii, kuimarisha mazingira ya biashara ya utalii kwa kuzingatia viwango vya afya na usalama vya kitaifa na kimataifa.

Pia kuboresha miundombinu katika maeneo ya vivutio vya utalii nchini, kutoa mafunzo kwa watoa huduma za utalii kuhusu namna ya kuendesha biashara za utalii hususani wakati wa majanga yanayotokea nchini.

Agosti mwaka jana aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Jaffar Haniu alitoa taarifa kwa vyombo vya habari iliyoeleza kuwa Rais Samia alianza kurekodi kipindi maarufu cha Royal Tour kwa ajili ya kuitangaza Tanzania kimataifa. Samia alirekodi kipindi hicho katika maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii na uwekezaji nchini na mafanikio yameanza kuonekana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live