Wakati matumizi ya nishati safi katika vyombo vya usafiri yakishika kasi duniani, Tanzania licha ya hatua ndogo iliyopiga ndiyo nchi kinara katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa na idadi kubwa ya vyombo hivyo vinavyotumia umeme.
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania, limeanzisha vituo vya kuchaji magari yatumiayo umeme Dodoma ili kuchochea zaidi mfumo huo.
Mtaalamu wa miradi wa UNDP Tanzania, Abbas Kitogo anasema data zilizopo zinaonyesha kuwa Tanzania inaongoza Afrika Mashariki katika matumizi ya magari na bajaji zinazotumia umeme, lakini kuna changamoto nyingi za kisera, kiteknolojia, kiuwekezaji, miundombinu na uelewa mdogo.
Kitogo anasema kwa sasa mradi huo upo katika hatua ya majaribio na hawafanyi biashara, bali kuhamasisha matumizi ya magari ya umeme.
Anasema kupitia kituo hicho, wawekezaji na wajasiriamali watajifunza na kupata uzoefu.
“Tumewekeza kwenye mradi huu kuhamasisha matumizi ya teknolojia nchini, ikiwamo kwa wawekezaji na wajasiriamali kujifunza na kupata uelewa.
“UNDP itaendelea kuwekeza katika kujenga uelewa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwamo sekta binafsi,” anasema Kitongo.
Pia, anasema shirika hilo linafikiria kupanga mradi mkubwa utakaoangalia miundombinu, ikiwamo kuongeza vituo kama hivyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
“Hivyo, kazi kubwa inatakiwa kufanyika kupunguza changamoto hizi. Tunaweza kusema bado Tanzania ipo katika hatua za mwanzo katika matumizi ya teknolojia hii,” anasema Kitongo.
Ripoti iitwayo E Mobility Alliance iliyotolewa Machi, 2023 ilionyesha kuwa idadi ya vyombo vya moto vitumiavyo umeme nchini ni takribani 5,000, lakini uchache wa vyombo hivyo unatokana na kodi kubwa katika bidhaa hizo, uelewa mdogo, mafundi wachache, watu kutokuwa karibu na umeme pamoja na kutokuwepo kwa sera za wazi kuhusu jambo hilo.
Ripoti hiyo inaonyesha hadi Februari 2023 Tanzania kulikuwa na kampuni 10 zinazojihusisha na uingizaji wa vipuri na vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme.
Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba alinukuliwa na gazeti la The Citizen akisema Serikali inafanya juhudi zote zinazowezekana kuvutia uwekezaji katika vyombo vya moto vitumiavyo umeme, lakini upatikanaji wa uhakika wa nishati hiyo muhimu ni mdogo.
Anasema kwa sasa Serikali ipo katika mpango wa kuandaa mkakati kwa ajili ya matumizi ya nishati safi katika vyombo vya moto.
“Tuko tayari kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha kunakuwa na vituo vya kutosha kwa ajili ya kuchaji vyombo vya moto vitumiavyo umeme,” anasema Mramba.
Kuhusu mapinduzi hayo yanayoendelea, Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu Dodoma (Udom), Dk Mwinuka Lutengano anasema ni vigumu kukimbilia teknolojia hizo za juu kama watu hawana uelewa wa kutosha.
Anasema kama wananchi na Serikali watakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu teknolojia ya kutumia umeme kuendesha vyombo vya moto kwa tija, kuna uwezekano mkubwa kuwepo kwa maboresho ya kisera.
Mtaalamu wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude anasema kuwepo kwa teknolojia ya e-mobility, ni jambo zuri kwa kuwa Serikali inataka kuhakikisha Tanzania inakuwa katika uchumi wa kijani.
“Mwanzoni kutakuwa na changamoto kadhaa kama kuwepo kwa huduma chache, lakini Serikali inatakiwa kuhakikisha kuna mifumo sahihi itakayosaidia kutoa elimu kuhusu umuhimu wa teknolojia husika,’’ anasema Mkude.
Pia, anasema kutokana na kuendelea kwa mapinduzi hayo na msukumo uliopo duniani, Serikali inatakiwa kuhakikisha kuna sera na viwanda vinavyotoa suluhisho la mahitaji muhimu yanayojitokeza.
Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar na Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja anasema ili teknolojia iweze kuendelea Serikali inatakiwa kuhakikisha kuna upatikanaji na matumizi sahihi ya nishati.
Historia magari ya umeme
Kuhusu matumizi ya umeme katika usafiri, historia inaeleza kwamba magari ya kwanza ya umeme yalianza kutumika kuanzia karne ya 19, lakini umaarufu wake ulipungua baadaye na magari yatumiayo mafuta yakashika soko kubwa.
Kwa sasa soko la vyombo vya usafiri duniani limebadilika sana, matumizi ya umeme yamekuwa yakipigiwa chapuo kila kona na uendelezaji wa vyombo vitumiavyo mafuta umepungua tofauti na miaka ya nyuma.
Kutokana na hilo, baadhi ya nchi zimeweka muda wa ukomo wa kuingiza magari yatumiayo mafuta na baadhi ya wazalishaji wakubwa wa magari wamepanga kuacha kuzalisha magari yatumiayo mafuta na kuhamia kwenye umeme.
Mpaka sasa inakadiriwa kuwa idadi ya magari yanayotumia umeme duniani ni zaidi ya milioni 14 na kutokana na mwenendo na mipango inayofanyika inakadiriwa kuwa hadi mwaka 2030 idadi hiyo itapanda hadi kufika milioni 43.
Baadhi ya mataifa makubwa yaliyoweka mbele suala la nishati safi hutumia umeme katika uendeshaji wa mabasi ya umma na treni, huku yakitoa motisha ya kikodi kwa watu binafsi wanaotaka kumiliki magari ya umeme.
Septemba mwaka jana ndege ya kwanza ya abiria ya kuchajiwa (inayotumia betri) ilifanya safari yake ya kwanza ya majaribio, endapo itaidhinishwa na vyombo vinavyodhibiti usafiri wa anga itaanza kutoa huduma.
Katika mwelekeo huohuo wa kuongezeka kwa matumizi ya nishati safi katika vyombo vya usafiri, madini yanahusika na utengenezaji wa betri zinazotunza umeme mwingi kwa muda mrefu bei yake katika soko la dunia imeongezeka na shughuli za uchimbaji na utafutaji zimeongezeka.
Vinara wa magari ya umeme
Mpaka Desemba 2022, Kampuni ya BYD Auto ya China ndiyo iliyokuwa inaongoza duniani kwa uzalishaji wa magari ya umeme kwa asilimia 20, ikifuatiwa na Tesla asilimia 12, Volkswagen asilimia 4, Wuling asilimia 3 na BMW asilimia 4.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Electric Vehicle Index mwaka 2021, China na Ujerumani ndizo nchi zilizokuwa mstari wa mbele katika matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme.
China ilikuwa nchi inayoongoza kwa maendeleo ya teknolojia ya magari yanayotumia umeme, huku Ujerumani ikipata alama za juu zaidi kulingana na mahitaji ya wateja.
Mataifa mengine vinara wa matumizi ya magari ya umeme ni Ufaransa, Marekani, Korea Kusini, Italia na Japan.
Kwa upande wa Bara la Afrika; Afrika Kusini ndio kinara, huku Mauritius, Shelisheli, Rwanda na nchi za Afrika Kaskazini ndizo zinazoongoza katika soko la magari hayo.