Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania kidijitali kupaisha utalii

769995251a8a3cb8bf805b41aeda347c Tanzania kidijitali kupaisha utalii

Wed, 17 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema kitendo cha Shirika la Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL) kuweka mawasiliano ya intaneti katika Mlima Kilimanjaro ni jambo la kihistoria kwa Tanzania na Afrika.

Nape alisema hayo jana katika kituo cha kupanda mlima huo cha Horombo wakati akizindua huduma ya mawasiliano ya intaneti katika mlima huo hivyo kuwezesha watalii kuwasiliana na wenzao wa maeneo mbalimbali duniani.

Alisema mlima huo mrefu zaidi Afrika ni moja ya vivutio bora zaidi duniani, ni fahari ya Tanzania na fahari ya Afrika.

“Kazi hii ikikamilika bila shaka itakuwa historia ya dunia na bila shaka tumekusudia kuiweka historia hiyo,” alisema Nape na akasema serikali inaendelea kufarijika kuona TTCL inashiriki kutatua changamoto za mawasiliano nchini.

Alisema awali watalii na watoa huduma za kitalii hawakuwa na mawasiliano wakati wanaupanda Mlima Kilimanjaro au kushuka na hata wakiwa mlimani.

“Hii ilikuwa hatari kwa usalama wa watalii na watoa huduma za kitalii. Aidha, kukosekana kwa mawasiliano serikali ilikuwa inakosa mapato sambamba na kuwanyima watalii kutangaza matukio mbalimbali ya kiutalii wakiwa katika Mlima Kilimanjaro. Kwa kuweka mawasiliano haya tunaweza tukapata mabalozi wengi sana wakatangaza mlima wetu bure bila sisi kuwalipa,” alisema Nape.

Alimshukuru Rais Samia kwa kufanya mapinduzi katika sekta ya utalii kupitia filamu ya Royal Tour na sasa nchi inanufaika na akabainisha kuwa kuna mafuriko na hekaheka ya watalii kwenye vituo vya utalii na viwanja vya ndege.

“Kwa uzinduzi wa intaneti hii sasa watalii wanaweza kupiga picha za mnato, video na mawasiliano mengine ya simu kwenda nchi mbalimbali duniani. Hii itaboresha sekta ya utalii, tuendeleze uboreshaji huu hadi kilele cha Uhuru kilichopo umbali wa meta 5,895 kutoka usawa wa bahari,” alisema Nape na kuongeza:

“Naambiwa hapa na watu wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) kwamba mlima huu unakuwa na takribani watalii 800 hadi 1,000 kwa siku wanapanda mlima….kubwa zaidi nathibitishiwa kwamba kuna watalii zaidi ya 6,000 kwa sasa katika mlima huu.”

Aliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), TTCL na Wizara ya Habari wahakikishe wageni wanaofika katika milango mikuu ya kuingia katika hifadhi nchini inakuwa na intaneti yenye kasi zaidi.

“Mara kadhaa nimesikia katika malango ya kuingia katika hifadhi na vivutio vya utalii wageni wanatumia muda mrefu kujisajili kutokana na mtandao kuwa chini, hili siyo sawa nategemea tutaondoa changamoto hii,” alisema.

Nape alisema kwa kufungwa kwa intaneti hiyo, watoa huduma za utalii wataboresha biashara zao lakini serikali itakusanya fedha za kigeni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo nchini.

Alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu kuhakikisha miundombinu ya mradi huo inalindwa.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Abdullah Mohamed alisema mradi huo utaimarisha usalama kwa watalii na waongoza watalii.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Peter Ulanga alisema juhudi za kupeleka huduma ya mawasiliano katika kituo cha Uhuru Peak kilichopo umbali wa Meta 5,895 zinafanyika na zinatarajiwa kukamilika kufikia Oktoba mwaka huu.

Alisema mradi huo umegharimu zaidi ya Sh mil 146 na kwamba umelenga kuhakikisha vituo vyote vya kupanda mlima huo vinakuwa na mawasiliano ya intaneti ya uhakika.

Naye Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, Anjela Nyaki amesema kuwekwa kwa mkongo wa mawasiliano ya huduma ya mawasiliano ya intaneti katika Mlima Kilimanjaro kutainua uchumi wa nchi na kuboresha usalama.

Alisema huduma hiyo itavutia wageni wengi kwenda kutalii katika Mlima huo kwa kuwa watalii watawasiliana na ndugu na jamaa moja kwa moja wakiwa mlimani.

Katibu wa Chama cha watoa huduma za Utalii Mkoa wa Arusha (TATO), Cyrili Ako alisema kuwekwa kwa mawasiliano katika Mlima Kilimanjaro ni jambo jema kwa nchi na watalii.

Ako alisema kumpa fursa mtalii kuwa na mawasiliano ya intaneti wakati akipanda mlima au akiwa mlimani kutampa faraja na kufanya ajisikie yupo nyumbani.

Hivi karibuni, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana alisema serikali

imejipanga kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini kufikia milioni tano ifikapo mwaka 2025.

Alisema wizara imedhamiria kuboresha mazingira ya uwekezaji ya biashara katika sekta ya utalii, ikiwa ni pamoja na kupunguza wingi wa usajili, tozo na malipo ya ada ya leseni.

Wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana alisema bungeni Dodoma kuwa, katika mwaka 2021, Tanzania imefanikiwa kupokea jumla ya watalii wa kimataifa 922,692 ikiwa ni ongezeko la asilimia 48.6 kutoka watalii 620,867 kwa mwaka 2020.

Aidha, aliwaeleza wabunge kuwa mapato yatokanayo na watalii wa kimataifa yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 714.59 mwaka 2020 hadi Dola za Marekani milioni 1,310.34 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 82.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live