Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania inatumia Tsh. Bilioni 10 kuagiza biskuti nje ya nchi

Hard Biscuit1 Ed Dr, Mpango ashangaa Tsh. Bilioni 10/- kuagiza biskuti nje

Sat, 9 Oct 2021 Chanzo: ippmedia.com

MAKAMU wa Rais, Dk. Phillip Mpango, amesema sekta ya viwanda imeshindwa kutengeneza bidhaa zinazokidhi mahitaji ya wananchi, huku akishangazwa na Sh. bilioni 9.8, kutumika kuagiza biskuti nje ya nchi.

Dr. Mpango amesema hayo wakati wa kukabidhi tuzo kwa mzalishaji bora wa mwaka, kwenye tuzo za Rais kwa Mzalishaji Bora wa Mwaka (PMAYA) zinazoandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI).

Mshindi wa jumla kwenye tuzo hizo, ilikuwa kampuni ya kiwanda cha Saruji cha Tanga,  mshindi wa pili Kampuni ya Bia ya TBL PLC na mshindi wa tatu kampuni za HANSPAUL.

Dk. Mpango alisema sekta ya viwanda ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya wananchi, lakini inasikitisha kuona bado inasuasua na kuagiza mawaziri husika kukutana na kuja na majibu ya uhakika.

“Bado tunaagiza bidhaa nyingi mno za viwandani na kwa kuagiza tunapeleka ajira nje ya nchi na kudidimiza viwanda vya ndani. CTI na wizara husika mkae mje na majibu ya namna gani tunaweza kutoka huko. Kuna  wenzetu walikuwa huko na wameshatoka, hivyo na ninyi mkutane na msije na majibu mepesi,” alisema Dk. Mpango.

Makamu wa Rais alitoa mfano kuwa mwaka jana pekee, zilitumika Sh. bilioni 200 kuagiza bidhaa za vitambaa wakati pamba inazalishwa kwa wingi nchini na Sh bilioni 111, zilitumika kuagiza bidhaa za sabuni.

Alisema Sh. bilioni 93, zilitumika kuagiza mafuta ghafi ya mawese, wakati mawese yanalimwa hapa hapa nchini, Sh. bilioni 33 bia zinazotokana na kimea wakati ngano, mahindi na shairi vinalimwa nchini.

Dk. Mpango alisema sekta ya viwanda ina jukumu la kuhakikisha inapenya zaidi, kwenye soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ile ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), ili kuongeza uuzaji wa bidhaa kwenye masoko hayo.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo alisema serikali inaendelea na jitihada za kuboresha mazingira ya biashara na malalamiko mengi ya wafanyabiashara yamepungua.

“Nilipoingia Wizara ya Viwanda (na Biashara) malalamiko yalikuwa mengi sana na CTI na washirika wake walikuwa hawakauki ofisini kwangu wakiwasilisha kero zao, lakini nikuhakikishie kwa sasa malalamiko yamepungua,” alisema Prof. Mkumbo.

Alisema kwa zaidi ya miaka minne, mauzo ya nje hayajawahi kupanda kuzidi Sh. bilioni moja, lakini kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Julai, mwaka huu, mauzo hayo, yameongezeka hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 1.1.

Mwenyekiti wa CTI, Paul Makanza, aliipongeza serikali kwa kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi ndani ya muda mfupi iliyokaa madarakani na kuviwezesha viwanda kufanya vizuri.

Alisema licha ya janga la corona, wenye viwanda wameonyesha ujasiri mkubwa kwa kuendelea na shughuli za uzalishaji wa bidhaa, wakati baadhi ya nchi zilishindwa na kufunga baadhi ya kazi zake.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, ambaye benki yake ni mfadhili mkuu wa PMAYA 2020, alisema uimara wa sekta ya fedha unategemea zaidi viwanda.

Alisema CRDB kwa kuona umuhimu wa sekta hiyo, imeshakopesha zaidi ya Sh. trilioni. 4.2 kwa wafanyabiashara wadogo na wakati, huku Sh. bilioni 815 zikielekezwa kwa wakulima na viwanda vidogo na vya kati.

Chanzo: ippmedia.com