Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania inajikokota kugharamia utafiti wa viwanda

18965 Pic+viwanda TanzaniaWeb

Mon, 24 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Baada ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kuandaa jukwaa la kwanza la fikra lililofanyika Juni likijadili magonjwa yasiyoambukiza, MCL inakuletea jukwaa la pili la fikra litakalofanyika katika ukumbi wa Kisenga, Kijitonyama, Oktoba 4, kujadili fursa na changamoto kuelekea Tanzania ya viwanda.

Wakati tukijiandaa kwa tukio hilo la kihistoria, tunakuletea mfululizo wa makala zinazobainisha fursa na kubainisha changamoto zilizopo. Leo tunakuletea maoni kuhusu mchango wa vyuo vya ufundi kufanikisha ndoto hiyo. Endelea...

Mwishoni mwa mwaka jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alitoa mwaka mmoja kwa kila mkoa kujenga walau viwanda 100 ili kuharakisha maendeleo na kuongeza upatikanaji wa ajira nchini.

Alitoa agizo hilo ukiwa ni utekelezaji wa kampeni ya ‘kiwanda change mkoa wangu’ inayowataka wakuu wa wilaya na mikoa kuweka mikakati ya kufanikisha lengo hilo.

Agizo la waziri huyu ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 utakaotegemea, kwa kiasi kikubwa, uzalishaji wa viwanda.

Mengi yanafanywa na Serikali hasa ujenzi wa miundombinu ya nishati, usafirishaji na uchukuzi hata Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) huku baadhi ya sera na sheria zikirekebishwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na ufanyaji biashara.

Tirdo

Hata hivyo, siyo rahisi kuzungumzia hata kujenga viwanda bila kufanya utafiti wa upatikanaji na ubora wa malighafi, teknolojia ya uzalishaji na uhakika wa masoko. Katika hili, umuhimu wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) lililoanzishwa Aprili Mosi, 1979 unajidhihirisha.

Mkurugenzi mkuu wa Tirdo, Profesa Mkumbukwa Mtambo anasema yapo maeneo matatu ya kipaumbele kuelekea uchumi imara chini ya sekta hiyo.

Kwanza, anasema ni rasilimali watu itakayotumika viwandani akitoa mfano wa sekta ya mafuta na gesi yenye uhaba wa watalaamu wazawa hatua inayozishawishi kampuni za kigeni kuwachukua kutoka nje.

“Pili ni muhimu kuwa na taarifa sahihi za maeneo ya uwekezaji. Kwa mfano unataka kuanzisha kiwanda cha chuma, ilimradi una pesa yako unakwenda kuanzisha kanda ya ziwa, malighafi isafirishwe hadi huko, utengeneze chuma huko halafu sehemu kubwa ya soko uilete tena Dar es Salaam,” anasema Profesa Mtambo.

Kukabiliana na changamoto ya kujenga kiwanda mbali na ama chanzo cha malighafi au soko, anasema shirika linafanya kazi na Mkoa wa Manyara kushughulikia suala hilo.

Lakini, anasema uanishaji wa maeneo ya viwanda (industrial mapping) inatakiwa ifanyike nchi nzima kujua mkoa unahitaji kuwa na viwanda vya aina gani kutokana na malighafi zilizopo.

Jambo jingine muhimu anasema ni uwezo wa kutabiri mahitaji ya teknolojia na soko kwa miaka ijayo. “Lazma tutazame mbele kujua miaka 15 ijayo ni viwanda gani vinakuja na vinahitaji malighafi gani ili tujiandae?” anasema.

Anasema nchi za Ulaya na Asia wameendelea kwa sababu hiyo hivyo Tanzania inapaswa teknolojia inayonunua sasa hivi itaendelea kuhitajika miaka 20 ijayo ili isije ikajikuta inaingiza mitambo ambayo ikatumika miaka mitano unaambiwa imepitwa na wakati hivyo kuingia gharama nyingine.

Anatoa mfano wa uwekezaji wa graphite ambao soko lake litakuwa kubwa kutokana na mapinduzi yanayofanywa kuachana na matumizi ya mafuta katika vyombo vya usafiri na kuhamia kwenye umeme.

Kutokana na hilo, anasema Serikali inaweza kufanya tathmini ya masoko na teknolojia katika rasilimali zilizopo nchini.

Bajeti ya utafiti

Kama ilivyo gharama kwenye ujenzi na uendeshaji wa viwanda, utafiti wake nao unahitaji fedha nyingi kuufanikisha kuifanya sekta hiyo kuwa endelevu.

Kutokana na ukweli huo, nchi nyingi duniani huwekeza fedha nyingi kuhakikisha zinafanya utafiti wa kina utakaozisaidia kushindana kwenye soko la kimataifa.

Mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga Sh10 bilioni kwa ajili ya utafiti unaoenda sambamba na hamasa ya ujenzi ya viwanda nchini.

Pamoja na kiasi hicho, takwimu za Tirdo za Machi 2016 zinaonyesha Tanzania ni nchi ya mwisho kwa ukubwa wa bajeti ya utafiti wa viwanda katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Utafiti huo unaonnyesha Kenya ipo juu zaidi kwa ukanda huu ikiwa na kiwango kikubwa zaidi ya Tanzania na Uganda zikiwekwa pamoja. Kumbukumbu zinaonyesha katika kipindi hicho, Shirika la Utafiti wa Viwanda Kenya (Kirdi) lilitumia Sh31.4 bilioni wakati Tanzania ikitumia Sh2.4 bilioni pekee.

Uganda kupitia shirika lake (Uiri) kwa upande wake ilitumia Sh8.7 bilioni. Kwa takwimu hizo, Tanzania ilizidiwa na majirani zake wote wawili. Wakati Kenya ikiizidi kwa zaidi ya mara 10, Uganda ilifanya hivyo kwa takriban mara nne. Kenya inatumia zaidi ya mara tatu ya bajeti ya Tanzania na Uganda kwa pamoja.

Hata nchi zilizoendelea, utafiti wa viwanda ni sehemu ya maeneo yanayopewa kipaumbele kikubwa kuyafanya yaendelee kuzalisha bidhaa bora kwa mahitaji ya ndani na nje pia.

Takwimu hizo za Tirdo zinaonyesha Singapore iliyokuwa na pato la Taifa (GDP) linalofika Dola 402 bilioni za Marekani ilitenga Dola 2.8 bilioni wakati Malaysia yenye GDP ya Dola 703 bilioni ikitenga Dola 47.2 milioni na India yenye GDP ya Dola 2.05 trilioni ikitumia Dola 250 kwenye utafiti wa viwanda.

Ripoti hiyo inabainisha changamoto zilizopo kwenye utengaji wa bajeti ya utafiti huo ikitaja kiasi kidogo kinachoidhinishwa na watunga sera, kutokuwapo kwa nia ya Serikali kuwekeza eneo hilo na uhaba wa watafiti.

Changamoto nyingine ni kukosekana kwa maabara za kutosha, madeni makubwa ya wazabuni na fedha kidogo za uendeshaji wa kila siku wa taasisi.

Kutokana na changamoto hizo, maeneo yanayoathirika zaidi ni idara ya utafiti wa sekta ya kilimo hasa viautilifu na mitambo, teknolojia ya chakula, usalama kazini, vifaa vya ufundi na uhandisi pamoja na mazingira.

Wadau

Kukosekana kwa fedha za kutosha kufanikisha utafiti wa viwanda ni suala linalowagusa wadau wengi wa maendeleo.

Mkurugenzi wa taasisi ya Repoa, Dk Abel Kinyondo anasema bila kutenga fedha za kutosha, kilimo cha kisasa hakitatokea hivyo bidhaa za Tanzania kamwe hazitoshindana kwenye soko la dunia kwa viwango vinavyokubalika.

Ofisa mtendaji mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), Moremi Marwa anasema ipo haja ya kuongeza vyanzo vya mapato kufanikisha utafiti unaokusudiwa kufanikisha uchumi wa viwanda Tanzania.

“Tuangalie vyanzo vingine licha ya hivi vilivyozoeleka,” anasema.

Chanzo: mwananchi.co.tz