Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania ina ukwasi wa kutosha- BoT

2bc330d81c6d23a39dbb2a7471730fa5 Majengo ya Benki Kuu ya Tanzania

Sat, 26 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania imeridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha katika kipindi cha Januari na Februari mwaka huu, uliowezesha uwepo wa ukwasi wa kutosha katika uchumi na utulivu wa viwango vya riba katika soko la fedha.

Pia kamati imesisitiza kuwa kutokana na mgogoro unaoendelea Ulaya Mashariki na hali ya mikwamo kwenye minyororo ya ugavi katika soko la dunia, itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa uchumi na kuchukua hatua stahiki pale itakapohitajika.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Benki Kuu Tanzania (BoT), kamati hiyo juzi ilifanya kikao chake cha kawaida cha 219 na kuidhinisha BoT kuendelea kutekeleza sera wezeshi ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi, ili kusaidia ukuaji zaidi wa mikopo kwa sekta binafsi na kuimarisha biashara na uwekezaji.

Ilibainisha kuwa mwenendo wa uchumi kwa mwaka 2021 ulikuwa wa kuridhisha na inatarajiwa ukuaji chanya kuendelea kwa mwaka 2022, kutokana na kuendelea kuimarika kwa shughuli za biashara na uwekezaji baada ya janga ya Covid-19.

Pia taarifa hiyo ilibainisha kuwa bidhaa na huduma zimepanda katika kipindi cha hivi karibuni, lakini mfumuko wa bei uliendelea kuwa ndani ya malengo ya asilimia 3-5 kwa upande wa Tanzania Bara na chini ya asilimia 5 kwa Zanzibar.

Ilieleza pia kuwa mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kuwa sawia na malengo kutokana na upatikanaji wa chakula cha kutosha na sera madhubuti za uchumi.

Athari zitokanazo na kupanda kwa bei ya nishati na bidhaa katika soko la dunia, hali inayochangiwa zaidi na mikwamo kwenye minyororo ya ugavi na mgogoro unaoendelea Ulaya Mashariki inaweza kusababisha kupanda kwa bei za bidhaa nchini.

Pia Kamati ya Sera ya Fedha imeridhishwa na kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ambayo imeendelea kuimarika hadi kufikia asilimia 11.9 mwezi Februari 2022.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live