Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania imepeleka Tumbaku nchi tatu kwaajili ya majaribio

41e07936c224c07cb092b2b390097873 Tanzania imepeleka Tumbaku nchi tatu kwaajili ya majaribio

Tue, 7 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI inaendelea na jitihada za kutafuta soko la tumbaku katika nchi mbalimbali hasa za Uarabuni, Afrika na Ulaya, bunge limeelezwa.

Kauli hiyo aliitoa Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe bungeni Dodoma jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta(CCM).

Sitta aliuza “Je, serikali ina mpango gani wa kuwezesha kampuni wazawa ili yawalipe wakulima mara wanaponunua tumbaku yao na kuhusu suala la kupata wanunuzi zaidi wa kununua tumbaku ni la muda mrefu. Je, kuna mafanikio yaliyopatikana?

Bashe alisema katika msimu 2020/21, nchi hii imefanikiwa kupata masoko mapya kwa kuuza tumbaku kwa majaribio nchini Romania (tani 200), Poland (tani 100) na Uturuki (tani 50).

Alisema sampuli za tumbaku zimetumwa China na Korea Kusini kwa ajili ya masoko hayo. Juhudi za kuirejesha kampuni ya TLTC zinaendelea na mwishoni mwa Septemba 2021, wizara itakutana uongozi wa kampuni hiyo.

Bashe alisema ni muhimu kama nchi kuendelea kulea kampuni za wazawa ili ziwe na uwezo wa kununua tumbaku kama kampuni za kigeni na kuunganisha kampuni za wazawa na taasisi za kifedha ili kupata huduma za kifedha.

Kwa muda mrefu biashara ya tumbaku imekuwa ikiendeshwa bila kampuni za kizawa kushiriki katika biashara ya tumbaku na kampuni za nje pekee ndizo zilikuwa zinashiriki katika biashara ya tumbaku.

Wakati wa ununuzi wa tumbaku kupitia kampuni za nje ununuzi wa tumbaku umeshuka hadi kufikia tani 42,000 za mkataba na baada ya kampuni za wazawa kuingia katika ununuzi, uzalishaji umeongeza kufikia tani 68,571 za tumbaku kupitia kilimo cha mkataba.

Katika masoko ya tumbaku msimu wa kilimo 2020/2021 jumla ya kampuni tisa zinanunua tumbaku ya wakulima zikiwemo kampuni saba za wazawa.

“Hata hivyo, kampuni hizo zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya kupata mitaji ya kutosha hali inayosabisha kuchelewa kuwalipa baadhi ya wakulima,”alisema.

Katika kutatua changamoto hiyo, Mei 2021 Wizara ya Kilimo ilikutanisha kampuni za wazawa na taasisi za fedha kwa lengo la kukubaliana na masharti nafuu yatakayowezesha kampuni hizo kupata mikopo kwa riba nafuu.

Mafanikio ya majadiliano hayo yameanza kupatikana ambapo Benki ya CRDB imeridhia kuzikopesha kampuni mbili za Mo Green International na Magefa Growers Limited.

Chanzo: www.habarileo.co.tz