Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania ilivyojipanga kuliteka soko la muhogo China

24333 Kilimo+pic TanzaniaWeb

Mon, 29 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanzania imejizatiti kulifufua zao la muhogo ili iweze kulikamata soko kubwa nchini China ambako kunatajwa kuwa yapo mahitaji makubwa ya kutosha kununua muhogo wote utakaozalishwa hapa nchini.

Kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya 12 kwa uzalishaji wa muhogo duniani na ya sita barani Afrika baada ya Nigeria, DRC, Ghana, Angola na Msumbiji ambapo uzalishaji wa muhogo kila mwaka unachangia asilimia 5.5 ya jumla ya uzalishaji duniani.

Hivi karibuni, wadau wa muhogo wakiwemo watunga sera, watafiti, sekta binafsi, wakulima na viongozi walikutana Jijini Dodoma kwa ajili ya kuendeleza mpango mkakati wa zao la muhogo kuwa la kibiashara na kuchangia katika pato la nchi.

Mkutano huo uliandaliwa na taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania (Tari), Taasisi ya kimataifa ya kilimo cha kitropiki (IITA) na Wizara ya Kilimo kitengo cha mpango wa maendeleo ya sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP II).

Mengi yalizungumzwa lakini kubwa likiwa ni mkakati wa kuliteka soko la muhogo katika taifa lenye watu wengi duniani la China. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Profesa Siza Tumbo aliamsha hisia za wajumbe kwa kueleza ukweli Tanzania inazalisha kidogo zao la muhogo na hivyo kushindwa kulikamata soko la China.

Profesa Tumbo alisema ni wakati wa wakulima kutumia fursa hiyo kwa haraka badala ya kuwa watazamaji na kuwaachia wenzao kutoka katika mataifa mengine ambao wakienda kwa kasi wanaweza kulishika soko hilo.

“Tatizo letu ni mitazamo hasi kutoka miongoni mwetu kwamba mazao ya asili kama mihogo na mtama eti hayafai kwa chakula, sasa kinyume chake tunashindwa kulishika soko kubwa ambalo liko wazi kwetu huo China,” alisema Profesa Tumbo.

Naibu alisema ni wakati wa wakulima kubadilika na kushindana zaidi ili kuachana na tabia ya kuwa wasindikizaji wa kila kitu hata vile vinavyowezekana.

“Sitaki kusikia kauli kama hizo, nataka watu walime muhogo, wale muhogo, wafanye biashara ya muhogo na si vinginevyo, lazima tufike mahali tuingie katika ushindani wenye tija,” anasema Profesa Tumbo. Anawataka wakulima wa muhogo kutokatishwa tamaa na kauli zinazotolewa, badala yake waongeze nguvu katika uzalishaji ili waweze kushindana na masoko makubwa ikiwemo nchi ya China.

Kwa mujibu wa wizara Tanzania imeshuka katika uzalishaji ukilinganisha na nchini zingine ambazo zimeongeza kasi ya kuzalishaji kama Brazil ambayo kwao muhogo umekuwa kama madini.

Mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania (TARI) Dk Geoffrey Mkamilo anasema muhogo ni zao la pili kwa umuhimu katika chakula baada ya mahindi ambapo asilimia 84 ya jumla ya uzalishaji nchini ni kwa matumizi ya chakula cha binadamu, lakini uzalishaji wake bado uko chini wakati zao halijatumika kikamilifu

Dk Mkamilo anasema mpango wa sasa ni kufanya mageuzi makubwa ya kulitoa zao la muhogo kutoka katika zao la chakula na kuwa zao la kibiashara ili kuwezesha pato la mkulima kukua.

Hesabu za mtaalamu huyo zinaonyesha kuwa, Tanzania inapaswa kuzalisha hadi tani 530,000 na 630,000 ili iweze kuuza nje lakini akasema kiwango cha uzalishaji kwa sasa ni kidogo zaidi licha ya kushindwa kusema ni kwa kiwango gain hasa.

Anasema mpango wa walioubuni utaendeleza teknolojia zilizothibitishwa na kupeleka mageuzi ya kutatua changamoto zinazowakabili wakulima ikiwemo uhaba mkubwa wa mbegu za kisasa.

Ameyataja maeneo yaliyopewa mkakati wa kuzalishajikwa wingi zao la muhogo ni kanda ya Ziwa, Mashariki na Kusini ambapo imebainika kuwa wanaweza kuzalisha kwa wingi zaidi licha ya maeneo yote kutakiwa kulima mhogo.

Wataalamu wanataja vitu vinavyotengenezwa kutokana na zao la muhogo ni unga, wanga na mali ghafi katika viwanda vya bia, pipi, vitafunwa, viwanda vya nguo, karatasi, rangi na madawa

Chanzo: mwananchi.co.tz