Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania huagiza tani 360,000 za mafuta ya kula nje ya nchi

13943 MAFUTA+PIC TanzaniaWeb

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba amesema Tanzania huagiza tani 360,000 za mafuta ya kula kutoka nje ya nchi kila mwaka.

Mgumba alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wadau wa zao la michikichi unaofanyika mkoani hapa.

Alisema kilimo cha michikichi kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa miche na mbegu bora.

Alibainisha kuwa mahitaji ya mafuta nchini ni zaidi ya tani 570,000 huku uzalishaji ukikadiriwa kuwa ni tani 210,000.

Alisema kiwango hicho ni cha mafuta yanayotokana na zao na mchikichi, ufuta, alizeti na mazao mengine.

“Tuna ardhi ya kutosha ya kuzalisha mafuta ndani ya nchi. Kukutana kwetu hapa ni kuleta tija, kuziainisha na kuzipatia ufumbuzi ili kuondokana na changamoto katika uzalishaji,” alisema.

Mkurugenzi wa taasisi ya Trade Mark East Africa (TMEA), John Ulanga alisema wadau katika mkutano huo wanapaswa kupanga mikakati wa namna ya kuleta mapinduzi katika zao la michikichi kwa maelezo kuwa tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa katika zao hilo kuna fursa nyingi.

Alisema majadiliano hayo pia yanaweza kuleta tija kwa wananchi kwa kuongeza kipato chao kwa kulima zao hilo.

“Soko la kwanza la mafuta yatokanayo na mchikichi liko ndani ya Tanzania. Ikiwa tutakuza zao hili tutaweza kukuza mazao mengine ya mafuta kutokana na unafuu wa bei utakaokuwepo,” alisema.

“Hata wafanyabiashara ambao wanaagiza mafuta nje ikiwezekana kuzalisha nchini na kuuza kwa bei nafuu nina amini wataanza kununua kwa wingi pamoja na kwamba tunajua kutakuwa na vikwazo lakini hatuna budi kukabiliana navyo,”alisema Ulanga.

Naye kaimu mtendaji mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Dk Sofia Kashenge alisema kuwa mkutano huo ni mwendelezo wa kazi iliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mkoani Kigoma alipokwenda kuhamasisha kilimo cha michikichi.

Alisema zao la michikichi katika programu ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP ll), liliongezewa uzito baada ya kuona matumizi ya mafuta ya mawese nchini na malighafi zinazotokana na zao la michikichi kuongezeka kwa kasi.

Alibainisha kuwa utafiti unaonyesha mpaka mwaka 2020 uhitaji wa mafuta ya mawese utaongezeka kwa kiwango kikubwa.

Alisema fursa zilizopo kwa sasa ni kuongeza uzalishaji wa zao hilo katika mikoa mingine mbali na Kigoma.

Dk Kasenge alisema suala la mbegu bado limekuwa ni changamoto kutokana na upatikanaji wake kutokuwa katika mtiririko maalumu na kwamba moja ya mkakati ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na mbegu bora kulingana na mazingira yaliyopo.

Chanzo: mwananchi.co.tz