Tanzania na Zambia (Tanzam) zinatarajia kusaini mkataba wa barabara ya njia nne kwa lengo la kupunguza ajali na msongamano wa magari kutoka Igawa Songwe hadi Mbeya vijijini yenye urefu wa kilometa 34.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili, Februari 12, 2023 Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa atashiriki katika hafla ya utiaji saini kati ya Wakala wa Barabara nchini (Tanroad) na Mkandarasi aliyepewa tenda itakayofanyika katika Stendi ya Mabasi ya Kabwe.
“Mradi huo ukianzia Wilaya ya Mbarali mpaka Mkoa wa Songwe utakuwa na urefu wa kilometa 218 ambapo suala la thamani na kujua mkandarasi aliyeshinda zabuni kati Kampuni nane zilizoshindanishwa itajulikana Februari 14, 2023 siku ya Jumanne.” amesema Homera.
Ameongeza kuwa miongoni mwa maboresho katika mradi huo ni pamoja na njia za pembezoni kwa ajili ya watembea kwa miguu ikiwepo usafiri wa pikipiki za matairi matatu (bajaji) lengo ni kuondokana na muingiliano wa vyombo vya moto.
Amesema uwepo wa mradi huo ni fursa kubwa kwa Watanzania na mataifa mengine kutumia Mkoa wa Mbeya kama lango la kiuchumi katika usafirishaji wa bidhaa kupeleka maeneo mbalimbali hususani mazao ya chakula na biashara.
“Nashukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali kwa Wizara ya ujenzi na Mawasiliano kusaini mkataba na kuanza utekelezaji wa mradi huu mkubwa ambao utapunguza ajali na msongamano wa magari makubwa yanayosafirisha mizigo kuja ndani na kutoka nje ya nchi.”amesema.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Masige Matari alisema upanuzi wa mradi wa barabara hizo itakuwa mwarobaini wa kupunguza msongamano wa magari na ajali za mara kwa mara.
“Mradi huu ni mkubwa wa kimkakati ambapo kwa wastani magari 1,300 kwa siku yatasafiri kupitia barabara hiyo jambo ambalo litachochea shughuli za kiuchumi kwa wanambeya na mataifa mengine.” Alisema Matari. Naye dereva wa masafa marefu, Jackson Amani amesema ni jambo jema la kujivunia uwepo wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mundombinu ya barabara hiyo ambayo ilikuwa ni changamoto kubwa kwao. “Tunaomba Wakuu wa Mikoa wa Songwe na Mbeya, kutusaidia madereva wa masafa marefu katika suala la wingi wa askari wa usalama barabarani kutokana na kukithiri kwa Rushwa aambavyo vinasababisha kuichukia Serikali.” alisema.