Serikali ya Tanzania na Uganda zimekubaliana kushirikiana katika kutatua vikwazo vya biashara ili kurahisisha shughuli hizo na kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo.
Makubaliano hayo yamefikiwa jijini Dar es Salaam jana, Mei 10, 2023 katika mkutano wa majadiliano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax na Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Rebecca Kadaga.
Akizungumzia hilo, Rebecca amesema kazi ya pamoja itafanyika kuhakikisha vikwazo vilivyopo katika itifaki ya soko la pamoja la forodha vinatatuliwa.
“Tuendelee kushirikiana kufanya kazi kwa pamoja ili kutatua vikwazo katika itifaki ya soko la pamoja la forodha,” amesema.
Hata hivyo, amesema mkutano huo umewawezesha kukamilisha baadhi ya mambo yaliyokuwa mezani na kujipa muda hadi mwishoni mwa Julai 2023 kukamilisha machache yaliyosalia.
Kwa upande wa Dk Tax amesema mataifa hayo yamekubaliana kujenga Kituo cha Uokoaji jijini Mwanza kitakachoshughulikia maafa yatakayotokea katika Ziwa Victoria
Kukamilika kwa kituo hicho, amesema kutarahisisha shughuli za uokoaji iwapo itatokea ajali yoyote katika Ziwa Victoria.
Makubaliano mengine ni kukamilisha ujenzi wa barabara na miundombinu mingine inayoziunganisha nchi hizo.
“Tumewekeana muda ili kukamilisha baadhi ya masuala kwa haraka lakini kuona jinsi gani pale panapohitaji kila nchi itoe rasilimali ijipange na kuhakikisha rasilimali hizo zinapatikana kwa wakati,” amesema.