Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania, Uganda kuboresha usafirishaji mizigo kupitia bandari

Bandari2 1 780x470nmnm Tanzania, Uganda kuboresha usafirishaji mizigo kupitia bandari

Fri, 1 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dar es Salaam. Nchi za Tanzania na Uganda zimeingia makubaliano ya kuongeza ufanisi wa usafirishaji mizigo inayotoka bandari ya Dar es Salaam kupitia ushoroba wa bandari za Ziwa Victoria kwenda nchi hiyo na nchi nyingine jirani.

Makubaliano hayo yameingiwa Dar es Salaam leo, Novemba 30, 2023 baada ya Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Uganda, General Edward Katumba kufanya kikao cha pamoja kilichowahusisha wataalamu wa sekta hizo kutoka mataifa hayo.

Akizungumza baada ya kikao hicho kilichodumu kwa saa tatu, Profesa Mbarawa amesema makubaliano hayo ni moja ya mkakati wa Serikali kuongeza idadi ya usafirishaji mizigo inayopitia bandari ya Dar es Salaam kwenda nje ya nchi kutoka asilimia mbili ya sasa hadi kufikia asilimia 15.

"Asilimia mbili maana yake ni mzigo tani 182,830 kwa sasa inapitia kwenye bandari ya Dar es Salaam ni kiwango kidogo. Tunaamini mikakati hii tuliyoipanga mzigo utaongezeka na ninatamani mzigo ufikie asilimia 15," amesema Profesa Mbarawa.

Amesema baada ya kuingia makubaliano hayo anatamani kuona mizigo yote inayoenda Uganda na mataifa mengine kwa asilimia 100 inapitia bandari ya Dar es Salaam.

"Sasa tunatoa siku 60 kwa mzigo wa Uganda kukaa bandari kavu ya Kwala bure, itavutia na kurahisisha wafanyabishara wengi wa Uganda kuagiza mizigo ya nje ya nchi kupitisha bandari ya Dar es Salam," amesema.

Katika makubaliano hayo, Profesa Mbarawa amegusia kuongeza vifaa kwa ajili ya usafirishaji mizigo kupitia kwenye reli.

"Madhumuni makubwa ya makubaliano haya ni kuzidisha ushirikiano wa usafirishaji kati ya Serikali ya Uganda na Tanzania kupitia bandari za ushoroba wa Mwanza," amesema.

Amesema Serikali zote mbili zimefanya jitihada za makusudi kuhakikisha kwamba zinaongeza kwa asilimia kubwa mzigo unaopitia bandari ya Dar es Salaam na kuwafanya wananchi wa mataifa yote kunufaika na rasilimali zilizopo.

"Kwa mfano hapa kwetu tumeandelea na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na wakandarasi wapo kwenye utekelezaji.

"Kwa upande wa usafirishaji kutoka Mwanza hadi Uganda, Serikali imefanya ukarabati mkubwa wa meli Mv Umoja ambayo tayari imeshaanza kufanya kazi," amesema.

Kwa upande wake, Waziri General Katumba amesema Uganda na Tanzania kupitia ushoroba wa Mwanza ni mpaka mzuri wa kufikia mataifa mengine ambayo ni Sudan Kusini, Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) yanayotumia bandari ya Dar es Salaam.

"Ni lazima ushoroba huo ufunguliwe kuwezesha shughuli za kibiashara hasa sekta binafsi zifanye kazi kwa masilahi mapana ya kukuza uchumi wa mataifa yetu," amesema.

Amesema Serikali hizo zimekutana kwa kuwahusisha wataalamu wa sekta ya uchukuzi kuja na mkakati wa pamoja kwa kuangalia namna ya kufungua ushoroba wa Mwanza.

"Ni jukumu letu kama mawaziri wa Uchukuzi kuangalia namna ya kufungua mpaka ili shughuli za kibiashara kwa jamii zetu zifanyike kwa ufasaha na uharaka kukidhi mahitaji ya masoko," amesema.

Amesema bado wanaheshimu hatua zilizoendelea Tanzania katika kuboresha bandari ya Dar es Salaam, lakini pia hata kuboresha bandari kavu ya Kwala kwa kuwawezesha mizigo kukaa siku hadi 60 bure.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live