Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania, Misri wajadili mradi Bwawa la Nyerere

Bwawa La Umeme Nyerere 780x470 1 Tanzania, Misri wajadili mradi Bwawa la Nyerere

Mon, 22 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nyumba, Nishati na Maendeleo ya Makazi wa Misri, Assem Elgazzar ambapo kikao hicho kilijikita kuzungumzia maendeleo ya mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao kwa sasa umefikia asilimia 95.83.

Mazungumzo hayo yamefanyika tarehe 21 Januari, 2024 jijini Dar es Salaam, ambapo Dk. Biteko ameeleza kuridhishwa kwake na kazi kubwa inayofanywa na Wakandarasi pamoja na TANESCO huku akieleza kufurahishwa kwake na taarifa iliyotolewa na Makamu wa Rais wa kampuni ya Elsewedy, Eng. Wael Hamdy ya kuwa majaribio ya mtambo namba 9 katika mradi wa JNHPP yameleta mafanikio na kilowati 100 zimeanza kuingizwa gridi ya Taifa.

Ameeleza kuwa, mafanikio ya majaribio hayo yanaleta matumaini kwani ratiba ya kazi inaenda mapema zaidi ya iliyopangwa mwanzo na hii ni kutokana na kazi nzuri ya Wakandarasi pamoja na TANESCO na kwamba lengo ni kuzalisha megawati 235 kutoka mtambo namba 9 ifikapo Februari mwaka huu na kuendelea na mitambo mingine ikiwemo mtambo Namba 8 na Namba 7.

Ameongeza kuwa, mradi huo ni wa kipaumbele cha Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan ili watanzania wapate umeme wa uhakika kwa kuwa mradi huo ukimalizika utaingiza megawati 2115 katika gridi ya Taifa.

Katika hatua nyingine, Dk. Biteko ameomba Watanzania wawe na subira wakati Serikali ikitekeleza miradi mbalimbali itakayoongeza kiasi cha umeme nchini ikiwemo mradi huo wa JNHPP.

Vilevile amesema kuwa, mradi wa JNHPP ni wa kielelezo kwa Afrika kwani inaonesha kuwa nchi za Kiafrika zinaweza zenyewe kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.

Kwa upande wake, Waziri wa Nyumba, Nishati na Maendeleo ya Makazi wa Misri, Assim Elgazzar amesema kuwa nia ya Serikali hiyo kutoka mwanzo ni kuona kuwa mradi huo unakamilika kwa ufanisi na kwa wakati na amewapongeza wakandarasi pamoja na TANESCO kwa hatua nzuri ya utekelezaji wa mradi huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live