Tanzania na Marekani wametia saini makubaliano ya Usafi ri Huru wa Anga baina ya nchi hizo ambao unatoa fursa ya ndege za abiria na mizigo za mataifa hayo kufanya safari za moja kwa moja kati yao.
Utiaji saini ulifanywa baina ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald Wright kwa niaba ya Serikali ya Marekani.
Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Mbarawa alisema hiyo ni hatua muhimu kwa sababu kusainiwa huko kunakwenda kufungua fursa za usafiri wa moja kwa moja kati ya mataifa hayo kwa abiria na mizigo.
“Ni hatua muhimu kwetu sote, makubaliano haya yanakwenda kufungua fursa lukuki zikiwemo za utalii na Marekani wana soko kubwa la utalii, maelekezo yangu kwa mamlaka zinazohusika na sekta ya usafiri wa anga kujipanga ili tuweze kufikia vigezo vya sisi kupeleka ndege zetu moja kwa moja Marekani,” alisema.
Profesa Mbarawa alisema kusainiwa kwa makubaliano hayo ni fursa pia kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kujipanga ili waweze kunufaika na mkataba huo kwa kuanzisha safari za moja kwa moja kwenda Marekani.
Akizungumzia mkataba huo, Balozi wa Marekani nchini, Donald Wright alisema makubaliano hayo yanafungua ukurasa mpya wa kuboresha na kuongeza wigo katika kuendesha mashirika ya ndege na kuongeza idadi ya safari baina ya mataifa hayo mawili.
Balozi Wright alisema makubaliano hayo yanafanya Wamarekani kuichagua Tanzania kama kituo cha utalii na pia kurahisisha wawekezaji wa Marekani kuja kuwekeza Tanzania kwa kuwa wanauhakika wa safari kupitia kampuni za ndege za mataifa hayo.
Akifafanua kuhusu mkataba huo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari alisema mkataba huo ni huru kwa mashirika ya ndege ya Tanzania kunufaika nao iwapo watapenda.
Alisema mkataba huo umezingatia mambo muhimu kadhaa yakiwemo usalama wa viwanja husika na usalama wa ndege na kusema kilichobaki sasa ni kupata ithibati ili kuruhusu ndege kuruka.