Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Marekani zimekubaliana kukuza uhusiano na ushirikiano katika Sekta ya Uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi nchini.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini, Michael Battle leo Agosti 15 Jijini Dodoma.
Viongozi hao pia wamejadiliana kuhusu namna ya kukuza uhusiano na ushirikiano wa uandaaji na utekelezaji wa mipango ya kiuchumi.
Aidha, wamekubaliana kuharakisha ukamilishaji wa Jukwaa la Majadiliano (Commercial Dialogue) baina ya Marekani na Tanzania ambalo litakuwa nguzo muhimu ya kuhamasisha Biashara na fursa za uwekezaji.
Waziri Mkumbo amemuhakikishia Balozi huyo wa Marekani kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini ili kukuza biashara na uwekezaji na amempongeza Balozi huyo kwa kuwa balozi mzuri wa kuitangaza vema Tanzania.