Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania, India kushirikiana viwanda vya mazao ya kilimo 

44486bdd6d33b7ab88187810cea8fe7c Tanzania, India kushirikiana viwanda vya mazao ya kilimo 

Sat, 17 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo, amesema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano na India katika maeneo ya kiuchumi ikiwamo uanzishwaji wa viwanda vya kuongezea thamani mazao.

Profesa Mkumbo aliyasema hayo wakati wa kuchangia kwenye mkutano wa biashara na uwekezaji kati ya India na nchi za Afrika uliofanyika kwa njia ya Mtandao, akimwakilisha Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.

Mkutano huo pia ulilenga kujadili jinsi India na nchi za Afrika zitakavyoweza kukuza ushirikiano katika kukuza uchumi kwa kuzingatia maeneo ambayo kila nchi ina vivutio zaidi vya kiuchumi.

Alisema serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na India katika maeneo ambayo yataongeza tija katika uchumi wa nchi kama vile kuanzisha viwanda vidogo vitakavyosaidia kuongeza thamani mazao yanayozalishwa nchini kabla ya kuuzwa katika nchini hiyo.

Profesa Mkumbo alisema Tanzania inatambua ushirikiano kati ya Tanzania na India na imeendelea kunufaika na ushirikiano huo hasa katika upatikanaji wa mikopo ya bei nafuu katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Profesa Mkumbo alitoa mfano wa baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Victoria kuyapeleka mkoani Tabora unaotarajiwa kunufaisha zaidi ya wakazi milioni moja wa wilaya za Nzega, Igunga, Uyui na Tabora mjini unaogharimu zaidi ya Sh bilioni 600.

Alisema Tanzania imeendelea kunufaika na masoko ya mazao ya aina mbalimbali kama vile korosho na mazao ya jamii ya kunde.

Mkumbo aliungana na mawaziri kutoka nchi nyingine za Afrika kuelezea utayari wa Tanzania kushiriki kikamilifu katika Makubaliano ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AFCFTA) ambao mchakato wake umefika katika hatua nzuri.

Pia alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji wa India kuja kuanzisha shughuli zao nchini ili wanufaike na soko hilo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa India na Afrika wakiwemo Makamu wa Rais wa nchi za Zimbabwe na Botswana.

Pia ulikutanisha mawaziri wenye dhamana za viwanda, biashara, uwekezaji, fedha, nishati, madini, kilimo na miundombinu kutoka nchi za Angola, Botswana, Burkina Faso, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Congo, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Guinea ya Ikweta, Eswatini, Ethiopia, Ghana, Kenya, Malawi, Mauntius, Morocco, Nigeria, Senega, Togo na Zimambwe.

Chanzo: www.habarileo.co.tz