Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania, Ethiopia zakubaliana kushirikiana kiuchumi

0f55d873cee0f4ebdc06a636a247ca9b.jpeg Tanzania, Ethiopia zakubaliana kushirikiana kiuchumi

Thu, 6 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tanzania na Ethiopia zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali, ikiwemo kiuchumi na amani.

Makubaliano hayo yalifikiwa katika mazungumzo baina ya Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Innocent Shiyo na Rais wa Ethiopia, Sahle- Work Zewde, wakati akiwasilisha hati za utambulisho kwa rais huyo jana.

Katika mazungumzo yao, Rais Zewde alimkaribisha Balozi Shiyo ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA) na kumpongeza kwa kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchini Ethiopia.

Aidha, alisifia uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Ethiopia uliojengwa na waasisi wa mataifa hayo mawili, Baba wa Taifa, Julius Nyerere na Mfalme Haile Selassie, ambao walifanya kazi pamoja kuanzisha Umoja wa Afrika.

Aliishukuru Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono Ethiopia kwenye masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa ikiwemo kwenye suala la matumizi ya maji ya Mto Nile chini ya ushirikiano wa Nchi za Bonde la Mto Nile.

Pia, aliipongeza Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya Ethiopia za kuhakikisha changamoto za usalama nchini Ethiopia zinapata ufumbuzi.

Pamoja na hayo, alimuahidi Balozi Shiyo ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake wakati wote atakapokuwepo nchini Ethiopia.

Kwa upande wake, Balozi Shiyo aliishukuru Serikali ya Ethiopia kwa mapokezi na ukarimu alioupata tangu kuwasili kwake nchini humo Novemba 26, mwaka huu.

Aidha, aliwasilisha salamu za heri kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwenda kwa Rais Zewde.

Balozi Shiyo alirejea mafanikio ya ziara ya Rais Zewde alioifanya nchini Januari mwaka jana ambapo nchi zote mbili zilikubaliana kuimarisha ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, uchukuzi, nishati, mifugo na bidhaa za ngozi, utalii, uhamiaji na ulinzi na usalama.

Pia, aliahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kwenye maeneo hayo na maeneo mengineyo yenye manufaa kwa pande zote mbili.

Vilevile aliongelea kuhusu suala la kuanza kufundisha lugha ya Kiswahili kwenye Chuo Kikuu cha Addis Ababa kupitia ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Addis Ababa.

Balozi Shiyo alimhakikishia rais huyo wa Ethiopia kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono nchi yake kwenye jithada za kurejesha amani na usalama nchini humo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live