Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kyaharara ameiongoza timu ya wataalamu kutoka nchini na konseli ya Tanzania katika kikao cha majadiliano kati ya Serikali Tanzania na Serikali ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kilichofanyika Lubumbashi nchini humo.
Kikao hicho cha siku mbili kilichomalizika jana Jumapili Aprili 28, 2024 ni mwendelezo wa utekelezaji wa makubaliano yaliyofanyika Julai 2022 katika mji wa Kalemie, Jimbo la Tanganyika, DRC, kuhusu uendelezaji na uendeshaji wa maeneo ya kimkakati kwa ajili ya bandari kavu ndani ya Tanzania na DRC.
Profesa Kyaharara amesema kikao cha makatibu wakuu kilikaa mara baada ya vikao vya wataalamu wa pande zote mbili ambao walikutana Aprili 25 na 26, 2024. Aidha, wataalamu hao wametembelea eneo la kimkakati litakalotumika kwa ajili ya usafirishaji wa shehena lililoko eneo la Kasumbalesa nchini humo.