Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatuma Almasi Nyangassa, ameiomba benki ya Tanzania Commercial Bank (TCB) kupanua wigo wa huduma zake katika wilaya hiyo ili kuwawezesha wajasiliamali kufikiwa huduma za kibenki na hivyo kupata fursa ya kujikwamua kiuchumi.
Nyangassa ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa tawi jipya na la kisasa la benki hiyo , lililopo karibu na Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kigamboni, ambalo ni sehemu ya mkakati wa kutimiza azma ya kitaifa ya kufikisha huduma za kifedha kwa kila mtanzania.
Amesema katika wilaya ya Kigamboni kuna wafanyabiashara na wajasiriamali wengi ambao wanahitaji huduma za kifedha, na akatumia fursa hiyo kuiomba benki ya TCB kuzidi kongeza na kuboresha miundombinu ya huduma zake ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
“ Wilaya yetu ya Kigamboni inazo shughuli nyingi za kiuchumi vikiwemo viwanda mbalimbali, vikubwa na vidogo, hivyo ujio wa benki hii ya TCB utarahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki na hivyo kuiunua ufanisi na ukuaji wa shughuli za uchumi,” alisema Fatma Nyangassa.
Akiongea katika hafla hiyo ya uzinduzi, Afisa Mtendaji Mkuu wa Tanzania Commercial Bank, Sabasaba Moshingi, alisema benki hiyo kwa sasa ni miongoni mwa benki kumi bora katika utoaji huduma hapa nchini, na kuwataka wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi katika tawi hilo kujipatia huduma mbali mbali, ikiwemo mikopo yenye riba nafuu.
Alisema Moshingi; “ Benki ya TCB pia inajali jamii hasa katika sekta za afya na elimu, na imewekeza katika kuhakikisha kuwa inaunga mkono program mbalimbali za sekta hizo muhimu ili kufanikisha azama ya serikali ya Awamu ya Sita kuinua kiwango cha maisha cha watanzania.
Moshingi amesema kuwa tawi la Kigamboni ni tawi la kwanza kwa wilaya hiyo, na kuongeza kuwa benki hiyo ina mtandao mpana nchini, ikiwa na inatoa huduma kupitia matawi mengine 82, na kuahidi kuwa TCB itaendelea kupanua wigo wa huduma zake ili kila mtanzania na mteja wa benki hiyo afikiwe na huduma na bidhaa mbalimbali zinazotolewa.