Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania, Algeria kushirikiana kwneye uchumi

Uchumi Kupanda Tanzania, Algeria kushirikiana kwneye uchumi

Mon, 31 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria zimesisitiza umuhimu wa kukuza diplomasia ya uchumi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Nchi hizo mbili ngazi ya Maafisa Waandamizi unaoendelea jijini Algiers, Algeria.

Mkutano huo ni maandalizi ya Mkutano Ngazi ya Mawaziri utakaofanyika tarehe 1 Agosti 2023 nchini humo ambapo ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unatarajiwa kuongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax (Mb.).

Ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya Maafisa Waandamizi umeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo. Viongozi wengine walioshiriki mkutano huo ni: Naibu Makatibu Wakuu kutoka sekta za Elimu, Sayansi na Teknolojia; Mambo ya Ndani ya Nchi, na Nishati.

Aidha, kwa upande wa Serikali ya Algeria, Mkutano huo ulifunguliwa na Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Selma Malika na kuhudhuriwa na Viongozi Waandamizi kutoka nchini humo.

Akifungua mkutano huo Balozi Shelukindo ameeleza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Algeria ni wa kihistoria na uliojengwa katika misingi imara na waasisi wa mataifa hayo mawili, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Ahmed Ben Bella.

Pia amesema Tanzania imejikita katika mageuzi ya kisekta hususan katika sekta za kilimo, utalii na taasisi za fedha ili kuiwezesha sekta binafsi kukuza uchumi wa Taifa. Pia inaendelea na ujenzi wa miundombinu ili kurahisisha mawasiliano kupitia usafiri wa barabara, reli, maji na anga.

‘’Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo wa kuimarisha sekta za uzalishaji na kuweka mpango wa usimamizi katika masuala ya biashara, uwekezaji na uchumi wa viwanda,’’ Alisema Balozi Shelukindo. Naye Balozi Selma Malika katika hotuba yake ameeleza kuwa mkutano huu wa tano unaonesha utayari wa pande zote mbili katika kukuza ushirikiano wenye tija kwa maslahi ya watu wake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live