Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tantrade kukuza mtandao soko la SADC

70201 Tan+pic

Wed, 7 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), imefungua milango kwa mjasiriamali yeyote kupeleka bidhaa zake kwa lengo la kukuza mtandao wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya Nchi 15 za Jumuiya ya Maendelo ya Kusini mwa Afrika(SADC).

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Agosti 6, 2019 Jijini Dar es Salaam nchini Tanzania ikiwa ni siku ya pili katika maonyesho ya bidhaa kupitia wiki ya viwanda kwa Nchi za jumuiya hiyo, yatakayofikia ukomo Ijumaa.

Katika maonyesho hayo, wafanyabiashara wa Tanzania wanayo mabanda 1,576 huku wageni wakiwa na mabanda 172 kutoka  nchi mbalimbali za jumuiya hiyo, wakitangaza bidhaa zao kwa lengo la kukuza mtandao wa soko na uzoefu kupitia maonyesho hayo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa mamlaka hiyo, Theresia Chilambo amesema mamlaka hiyo tayari inaendelea kupanua mtandao wa masoko ya Tanzania ndani ya nchi hizo, akitolea mfano wa wafanyabiashara waliopata masoko Msumbiji na Eswatini kupitia ushirikiano wa Tantrade.

“Kuna Kampuni ya Bakhresa ilipata masoko kwa mara ya kwanza mwaka 2008 nchini Msumbiji baada ya kuwapeleka katika maonyesho ya biashara,” alisema Theresa

Maonyesho hayo kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka 2016 nchini Eswatini, mwaka 2017 nchini Afrika Kusini , mwaka 2017 nchini Namibia na awamu ya nne mwaka huu nchini Tanzania ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa awamu ya kwanza 2015/30 ya Mkakati wa Viwanda wa SADC 2015/2063.

Pia Soma

Theresa amesema milango iko wazi kwa ajili ya kusaidia kutangaza na kutafuta masoko kwa wajasiriamali wa ndani kupitia usajili wa maonyesho ya kila mwaka ya Sabasaba.

“Lakini pia Tantrade ni mwanachama wa Shirikisho la Kimataifa la Maonyesho Duniani (UFI) kwa hiyo kila mwaka tunaangalia bidhaa gani za Tanzania tunaweza kuzipeleka katika maonyesho ya  nchi za SADC na Afrika Mashariki,” amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz