Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanoil yapata hasara Sh7.83 bilioni

Mafuta Pic Data (2) Tanoil yapata hasara Sh7.83 bilioni

Thu, 15 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imesema Kampuni ya Mafuta ya Tanoil imepata hasara ya Sh166 milioni mwaka 2020/21 hadi kufikia Sh7.83 bilioni.

Kamati hiyo imesema ongezeko hilo limesababishwa na kampuni hiyo ambayo ni ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kuuza mafuta kwa bei ya chini ya ile iliyopangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).

Mwenyekiti wa PIC, Deus Sangu amesema hayo jana Februari 14, 2024 wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati hiyo kwa mwaka 2023.

Sangu amesema kukosekana kwa usimamizi madhubuti wa kampuni tanzu, baadhi ya kampuni zimekuwa zikizianzisha kampuni tanzu bila kufuata muongozo uliowekwa na msajili wa hazina.

Amesema jambo hilo limesababisha na usimamizi kutokuwa mzuri, hivyo kukosekana kwa ufanisi na tija ya uwekezaji.

Sangu amesema uchambuzi wa kamati umebaini dosari katika usimamizi wa mtaji wa umma uliowekezwa Tanoil na kumepewa jukumu la uagizaji na usambazaji wa nishati ya mafuta.

Amesema dosari zilizobainika ni pamoja na kukua kwa madeni ya muda mfupi ya kampuni kwa asilimia zaidi ya 100 kutoka Sh6.8 bilioni mwaka 2020/21 kufikia Sh30.0 bilioni mwaka 2021/22, ongezeko hilo ni la zaidi ya asilimia 100.

Sangu ambaye ni mbunge wa Kwela, amesema kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo kampuni imekuwa ikipata hasara kutoka Sh166 milioni mwaka 2020/21 hadi kufikia Sh7.83 bilioni.

“Hasara hii kwa kiasi kikubwa imesababishwa na kuuza mafuta kwa bei ya chini ya bei iliyopangwa na Ewura,” amesema Sangu.

Pia, amesema kwa msingi huo, kamati inaona ni muhimu uwekwe utaratibu wa Serikali kuhakikisha msajili wa hazina anashirikishwa katika hatua zote za uanzishaji, uwekaji wa mtaji na uendeshaji wa biashara zinazofanywa na kampuni tanzu.

Aeshi aibua mgogoro

Katika hatua nyingine, mbunge wa Sumbawanga Aeshi Hilaly ameitaka Serikali kuchunguza mgogoro wa ardhi wa Shamba la Mzindakaya ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kama yaliyotokea katika shamba la Mzindakaya lililopo Wilaya ya Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa.

Shamba hilo lilikuwa likimilikiwa na mwanasiasa maarufu aliyeshika nafasi mbalimbali serikalini ikiwamo ukuu wa mikoa katika awamu ya kwanza, Christian Mzindakaya aliyefariki dunia Juni 7, mwaka 2021.

Mgogoro wa shamba hilo unakuja huku kukiwa na mgogoro mwingine wa muda mrefu kati ya wananchi na Kanisa la Efatha lililopo Kijiji cha Sikaunga, wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa.

Novemba mwaka jana, ziliibuka vurugu katika shamba hilo, watu wawili walijeruhiwa baada ya kutokea mgogoro kati ya walinzi na wananchi uliosababishwa na baadhi ya watu kuchunga mifugo na kulima kwenye shamba hilo.

Akichangia katika taarifa ya shughuli za Kamati ya PIC, Aeshi amesema shamba la Mzindakaya alilipata kupitia mkopo wa Benki Kuu.

Amesema alisimamia shamba kwa muda mrefu lakini kwa bahati mbaya riba na faini za mkopo huo zilifanya mkopo kufikia Sh28 bilioni.

“TIB (Benki ya Maendeleo Tanzania) wakaazimia kuliuza shamba hilo, benki hiyo wamekaa chini na kutoa penalty (faini) na riba zote, hatimaye lilishuka hadi Sh14 bilioni,” amesema.

Amesema Wizara ya Kilimo iliandikia barua Benki ya TIB kuwa iko tayari kulinunua shamba hilo kwa Sh14 bilioni kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu na kilimo cha ngano.

Hata hivyo, Aeshi amesema wajanja wameenda kununua shamba hilo kwa Sh2 bilioni na kiasi kilichobaki wamekubaliana na benki hiyo kuwa watalipa kidogo kidogo.

Amehoji kama kuna fursa ya kulipa kidogo kidogo kwa nini wasingeacha kwa familia ya Mzindakaya waanze kulipa taratibu hadi kiasi hicho kimalizike.

“Najiuliza kulikuwa na haja gani ya kuuza shamba hilo kwa Sh2 bilioni, Waziri (Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba) saa nyingine tukisimama hapa tunasimama kwa uchungu. Tukihoji katika kamati kuna maneno yanakuja kuja ohoo ni maelekezo. Ni nani anatoa maelekezo hayo mtuambie,” amehoji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live