Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tani nyingine 4,600 za Mahindi zimenunuliwa na NFRA

E6b8b1a31f90f2cc9f839ca0250b9f2f Tani nyingine 4,600 za Mahindi zimenunuliwa na NFRA

Thu, 2 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAKALA wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imenunua tani 4,600 za mahindi zenye thamani ya Sh bilioni 2.3 kutoka kwa wakulima mkoani Rukwa.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Hifadhi ya Chakula, Milton Lupa amesema NFRA ilipanga kununua tani 5,000 Agosti 31, mwaka huu.

Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti ofisini kwake Sumbawanga wakati wa ziara ya kukagua zoezi la ununuzi wa mahindi meupe linaloendelea mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Lupa amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kununua mahindi kulingana na upatikanaji wa fedha.

“Wakala unaendelea kufuatilia fedha toka Serikalini ili itekeleze jukumu la kununua mahindi kama ilivyopangwa kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022 hivyo wananchi wa Rukwa wawe na subira” alisema Lupa.

Aidha, alisema kuwa wakala unaendelea kukamilisha ujenzi wa vihenge vya kisasa na kuwa lengo mahindi yote yatakayonunuliwa Rukwa msimu huu yahifadhiwe.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti alisema wananchi wa Rukwa wamezalisha kwa wingi mahindi kwa kuwa ni zao lao la biashara hivyo wanategemea zaidi NFRA kama soko la uhahika.

“Tunaendelea kuiomba Serikali itupatie mgao zaidi sisi wana Rukwa kwani zao letu la mahindi ndio zao la biashara kwa wananchi wengi” alisisitiza Mkirikiti.

Kwa mujibu wa takwimu za uzalishaji wa mazao ya chakula, kilimo msimu wa 2020/2021 Mkoa wa Rukwa ulizalisha tani 651,433 za mahindi kati ya lengo la tani 731,500 ambapo kutokana na uzalishaji mkubwa Mkoa umepata ziada ya tani 354,117.

Chanzo: www.habarileo.co.tz