Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tani 80,000 za sukari iliyoagizwa nje ya nchi zakwama kuuzika

11353 Sukari+pic TanzaniaWeb

Sat, 14 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Zaidi ya tani 80,000 za sukari kati ya 130,000 zilizoagizwa na wazalishaji wa hapa nchini, zimekosa soko kutokana na wingi wa bidhaa hiyo inayoigizwa kwa magendo.

Sukari hiyo iliagizwa kati ya Machi na Juni ili kuziba pengo la mahitaji ya bidhaa hiyo wakati viwanda vya ndani vinaposimamisha uzalishaji.

Mkurugenzi wa Chama cha Wazalishaji wa Sukari nchini, Seif Ali Seif aliiomba Serikali jana kuongeza mapambano dhidi ya watu wanaoingiza sukari nchini kinyume cha utaratibu.

Seif alisema katika uagizaji wa sukari kuna makundi mawili wakiwamo wale wanaoagiza kinyume cha sheria na wanaoagiza za viwandani na kuiuza kwa matumizi ya nyumbani. “Sukari ya viwandani ina madhara kwa matumizi ya nyumbani, tukiruhusu sukari hii ikaingia nchini kwetu itasababisha madhara makubwa kwa wananchi. Wananchi watoe ushirikiano kwa kutoa taarifa waonapo sukari hiyo sokoni,” alisema.

Aliwataka wananchi wanunue vitu vyenye ubora vinavyozalishwa nchini ili kuepusha madhara ya matumizi ya sukari inayoingizwa kimagendo.

Seif alisema hali ya udhibiti wa sukari kwa sasa inaridhisha baada ya Serikali kuingilia kati na kuwapa jukumu wazalishaji kuagiza sukari.

Hata hivyo, alisema wanahitaji jitihada ziongezwe zaidi kwa sababu bado sukari ipo nyingi mitaani.

“Kuna wengine wanaingiza sukari nchini na kuzifunga kwa kutumia vifungashio vinavyofanana na vile vya wazalishaji wa ndani. Tumetembelea baadhi ya maduka na kukuta sukari hizo zinauzwa,” alisema Seif.

Mkurugenzi wa masoko na uendeshaji wa Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa, Fulgence Bube alisema sukari ya viwandani inapouzwa kwa matumizi ya nyumbani siyo tu ina madhara kwa binadamu, bali pia Serikali inakosa mapato.

Sukari ya viwandani hutumika kutengenezea vyakula, vinywaji na dawa.

Chanzo: mwananchi.co.tz