Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tani 30 mahindi ya msaada zapelekwa Kahama

Maguni Ya Mahindi Tani 30 mahindi ya msaada zapelekwa Kahama

Mon, 9 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mbunge wa Kahama Mjini, mkoani Shinyanga, Jumanne Kishimba amesema zitaletwa tani 30 za mahindi ya msaada kutoka Wakala ya Taifa ya Hifadhi ya Chakula (NFRA) na kuwauzia wananchi kwa bei nafuu.

Kishimba alisema hayo jana kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika kwa nyakati tofauti kwenye kata za Malunga na Mhongolo.

Alisema kilio cha wananchi kimesikika baada ya bei za vyakula kuwa juu yakiwamo mahindi hivyo serikali imeona changamoto hiyo na kuitatua kwa kuleta mahindi.

“Tayari mazungumzo yamefanyika na NFRA kwa Kahama Mjini zitaletwa tani 30 za mahindi na kuuzwa kwa bei nafuu,” alisema Kishimba.

Baadhi ya wananchi wa Mjini Kahama, Joackimu Samweli na Magdalena Issa walisema changamoto ipo kwenye bei ya vyakula na kuwa debe moja la mahindi wanauziwa Sh 22,000.

Meneja wa NFRA, Kanda ya Shinyanga, Joseph Maige alikiri tani hizo za mahindi kupelekwa Kahama kuanzia leo ili kupunguza makali ya bei ya mahindi na zitaendelea kupelekwa zaidi ya hizo.

Maige alisema kanda hiyo inajumuisha mikoa minane ya Kigoma, Kagera, Mara, Simiyu, Geita, Tabora, Mwanza na Shinyanga na serikali imejipanga maeneo yote kuwapelekea mahindi hayo na bei elekezi itapangwa.

“Wataendelea kutoa mahindi hayo kwa sababu ya kupanda kwa bei ya mahindi na wananchi wa hali ya chini kushindwa kumudu bei zilizopo sokoni sasa,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live