Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tani 130 za mchele zapigwa marufuku kuingizwa sokoni

Mchele Nchi Jirani Tani 130 za mchele zapigwa marufuku kuingizwa sokoni

Sun, 12 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tani 130 za mchele wa Kampuni ya Sahal General Store Zanzibar zimeharibika moja ya sababu ikidaiwa ni kukaa kwenye makontena bandarini muda mrefu bila kushushwa.

Tani hizo zimebainika jana Machi 11, 2023 baada ya kampuni hiyo kuhisi kuharibika kwa mchele huo na kutoa taarifa kwa Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) ili kufanya ukaguzi katika ghala hilo lililopo Malindi Unguja na kukuta mchele huo kutoka Pakistan ukiwa na wadudu na kubadilika rangi.

Ofisa kutoka TFDA, Mohammed Shauri amepiga marufuku mchele huo kuingizwa sokoni huku sababu ya kuharibika pia ikielezwa ni kujazwa bidhaa nyingi kwenye kontena hivyo kukosekana hewa na kusababisha joto kali.

“Niwashauri wafanyabiashara kufuata taratibu mapema ili kuepusha bidhaa zao kukaa muda mrefu ndani ya makontena kunakosababisha kuharibika kwa bidhaa hizo na kusababisha hasara kwao na madhara kwa jamii,” amesema.

Pia amewataka wafanyabiashara kuacha kuingiza bidhaa sokoni pindi wanapobaini dalili za kuharibika kwa bidhaa husika badala yake kufika ZFDA kwa ajili ya ukaguzi ili kuepusha madhara yanayoweza kuepukika.

Mapema Ofisa kutoka ZFDA aliitaka kampuni hiyo ya Sahal General Store kufuata taratibu watakazopewa na ZFDA ili kuuteketeza mchele huo maana unaweza kusababisha madhara makubwa kwa jamii.

Naye Mkuu wa utoaji wa mizigo bandarini katika Kampuni ya Sahal General Store, Juma Abubakar Alhaji alisema kuharibika kwa mchele huo kumechangiwa na joto lililosababishwa na ukaaji wa muda mrefu bandarini.

Hivyo ameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya bandari ili kuepusha msongamano wa meli za makontena bandarini kunakosababisha kuchelewa kushushwa kwa makontena.

Juma amsema wapo tayari kushirikiana na Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar kuhakikisha mchele huo hautumiwi na binadamu kwani wapo kwaajili ya kulinda afya zao na siyo vinginevyo.

Amesema mchele huo ulipakiwa kutoka Pakistan Novemba 15, 2022 na ukafika bandarini ya Zanzibar Januari 8, 2023 lakini umeshushwa bandarini Machi 9, 2023.

"Ungetolewa mapema hali hiyo isingetokea kwa hiyo tunalalamika kwa banadari kuchelewa kushushwa, tunaomba serikali itusaidie meli zinapofika hapa meli zishushe mizigo," amesema.

Ukaguzi wa ZFDA umefanyika kufuatia Kampuni ya Sahal General Store kujisalimisha baada ya kubaini mchele huo walioingiza haufai kwa matumizi ya binadamu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live