Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanga waonja neema upatikanaji sukari

SUKARI Tanga waonja neema upatikanaji sukari

Tue, 19 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

UPATIKANAJI wa sukari mkoani Tanga umerejea katika hali yake ya kawaida katika maeneo mbalimbali.

Wiki mbili zilizopita wananchi katika maeneo mengi nchini walikutana na machungu na shubiri kutokana na kuadimika kwa bidhaa hiyo muhimu.

Wafanyabiashara wengi walitumia uhaba huo kwa kuificha kisha kuiuza kwa bei ya juu.

Katika Jiji la Tanga maduka yote ya jumla na rejareja sasa yana bidhaa hiyo, huku tofauti kubwa ikiwa ni kwenye bei.

Maduka mengi ya jumla yanauza kati Sh. 2,900 hadi 3,200 kwa kilo moja wakati maduka ya rejareja yenyewe kilo moja ikiuzwa kati ya Sh. 3,600 hadi 4,000.

Baadhi ya wafanyabiashara wa jumla na rejareja wa eneo la barabara la 15 lenye maduka mengi waliieleza Nipashe kuwa upatikanaji wa bidhaa umeanza kutengemaa, hivyo bei itakuwa inashuka kutokana na mzunguko wa biashara.

Ally Ndahani, alisema mwishoni mwa wiki walianza kupata bidhaa hiyo, lakini ni vigumu kudhibiti bei kwa haraka.

"Huu ni mzunguko wa biashara huwezi kuudhibiti bei kwa haraka, haiwezekani kabisa duniani kote… bei itaendelea kushuka taratibu kutokana na upatikanaji wa sukari kwa mawakala wetu,” alisema Ndahani.

Katika mitaa mingi ya Jiji la Tanga hususani maeneo maarufu kama Sahare, Nguvumali, Pongwe Kange, Donge na Raskazone, bidhaa hiyo inapatikana kwa urahisi zaidi huku kilio kikubwa kwa wananchi ni kutokana na bei kubwa ya sukari.

Ashura Kachenje, mkazi wa Nguvumali, alisema wanashukuru kuona hali ya upatikanaji wa sukari kurejea kama awali.

“Sisi tunashukuru kwa upatikanaji, tuliteseka sana wiki mbili hizi, lakini tunaomba bei ipunguzwe ili tumudu kununua, kama unavyoona hapa. Nimetoka kununua hii ni robo nimeuziwa shilingi 1,000 huoni hili ni tatizo," alisema Ashura.

Katika wilaya mbalimbali za mkoa wa Tanga, bidhaa hiyo imeanza kupatikana ambapo katika wilaya za Mkinga, Pangani na Muheza, sukari inapatikana katika maduka mengi, huku changamoto ikiwa ni bei kubwa kati ya shilingi 3,600 na 4,000.

Katika wilaya za Handeni, Kilindi, Korogwe na Lushoto, hali ya upatikanaji imeendelea kuimarika, lakini bei ikiendelea kuwa tatizo kutokana na kuuzwa kati ya shilingi 3,200 na 4,500 kwa kilo moja hususani katika wilaya za Kilindi na Lushoto.

Katika Wilaya ya Korogwe kilo moja inauzwa kati ya shilingi 2,700 na 2,800 katika eneo la Manundu lililopo Korogwe Mjini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live