SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) litapeleka mtambo wa umeme wa Megawati 20 mkoani Mtwara kutoka kituo cha umeme 'Ubungo III' ili kuimarisha hali ya umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara ikiwa ni utekelezaji wa agizo alilolitoa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko kwa TANESCO la kuimarisha hali ya umeme katika mikoa hiyo.
Agizo hilo la kuimarisha hali ya umeme katika Mikoa ya Lindi na Mtwara alilitoa wakati alipofanya ziara ya kikazi katika mikoa hiyo na kukuta hali isiyoridhisha ya upatikanaji umeme.
Hayo yamebainika wakati wa kikao cha Dk. Doto Biteko na Bodi pamoja na Menejimenti ya TANESCO kilichofanyika jana jijini Dodoma.
Aidha, Dk. Biteko ameiagiza TANESCO kuongeza nguvu katika kutekeleza miradi ya uzalishaji umeme nchini kwa kutumia fedha zilizopo ili nchi iweze kuwa na umeme wa kutosha kusambazia wananchi ikiwemo umeme kutoka katika vyanzo vya nishati jadidifu.
Kiongozi huyo pia ameitaka Bodi ya TANESCO kulisimamia vyema Shirika hilo na wafanye kazi kwa kushirikiana na Menejimenti kwani lengo la Shirika hilo ni kuhakiksha kunakuwa na umeme wa kutosha kwa matumizi mbalimbali.
Amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-hanga kusimamia na kuwatumia Watendaji na Wataalam wa shirika hilo vizuri ili kuwe na ufanisi katika shughuli zao za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme.
Dk. Biteko ameitaka TANESCO pia kuboresha Kitengo cha Huduma kwa Mteja kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwaendeleza wataalam wanaotoa huduma kwa wananchi ili watoe huduma bora na yeye ameahidi kutoa ushirikiano kwa Shirika hilo pale utakapohitajika.
Dk. Biteko pia, ameitaka Bodi ya TANESCO kutokuwa na urasimu katika ufanyaji wa maamuzi na uzito wa kufuatilia masuala mbalimbali ili kutochelewesha miradi mbalimbali ya umeme.