Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanesco kununua umeme wa Aqua

Umeme 1 Tanesco kununua umeme wa Aqua

Mon, 26 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya kuongeza nguvu kwenye gridi ya Taifa ambayo hivi karibuni Mkoa wa Kigoma uliunganishwa, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema lipo tayari kununua megawati 45 zinazozalishwa na kampuni ya Aqua Power Tanzania Limited mkoani Mtwara.

Kampuni hiyo ambayo kwa sasa imesimamisha uzalishaji na inatafuta mnunuzi wa kuiendesha mitambo hiyo, ina kiwanda cha kuzalisha umeme unaotokana na gesi asilia.

Mkurugenzi wa Mipango wa Tanesco, John Mageni alipoulizwa kama Tanesco itakuwa tayari kuinunua na kuendesha mitambo hiyo, alisema: “Kanuni za ununuzi haziiruhusu Tanesco kununua mashine zilizotumika.

Kama shirika la Serikali, tunatakiwa kununua mitambo mipya lakini mtu binafsi au kampuni inaweza kununua na kuendesha mtambo huo, Tanesco iko tayari kununua umeme utakaozalishwa.”

Aidha, Mageni alisema Tanesco itakubali kuingia mkataba wa kununua umeme unaozalishwa na mitambo hiyo endapo wataona bei inafaa.

“Kama bei itakuwa rafiki tuko tayari kununua umeme kutoka kwao ili tuendelee kuongeza nguvu kwenye gridi ya Taifa,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Maharage Chande alisema uchunguzi wa kina unahitajika kabla ya kuinunua mitambo hiyo.

“Tutahitaji kuchunguza uwezo wa mtambo, saa za uendeshaji na mwendo wake, endapo majibu yakiridhisha basi suala hilo litapelekwa kwa uongozi,” alisema Chande.

Aidha, Chande alisema menejimenti itaomba idhini kutoka kwa bodi ambayo italazimika kuidhinishwa na wizara inayohusika na nishati.

“Ni mchakato, udhibiti wa ununuzi bila shaka haupendekezi mali iliyotumika, lakini siwezi kusema kwani mchakato unahitaji kuzingatiwa,” aliongeza.

Wakili Adrounicus Byamungu, kaimu meneja wa kampuni ya Aqua Power, alisema: “Ni sawa na kusema mtambo ni mpya kwa sababu ulifanya kazi kwa miaka miwili tu.”

Byamungu alisema kiwanda hicho kiliacha kufanya kazi baada ya kampuni ya Dangote kuacha kununua megawati zote 45 za umeme inazozalisha.

“Sasa tunatafuta mmiliki mpya ambaye anakwenda kuiuzia Tanesco umeme huo, megawati 45 ni umeme mkubwa, kwa kweli uwezo huu ni zaidi ya nusu ya Bwawa la Mtera,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live