BODI ya Utalii Tanzania (TTB) na Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato) wamelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kwa ubunifu wa kulipa ili kumpa faru jina lako na pia kuasili wanyama.
Hivi karibuni Tanapa ilitangaza kuanzisha programu ya kutoa jina la mtu kwa faru kwa gharama ya Sh milioni tano.
Kamishna wa Uhifadhi, William Mwakilema alisema Dodoma kuwa Bodi ya Wadhamini ya Tanapa imeshaipitisha programu hiyo na kuanzia sasa mtu akitaka kutoa jina kwa faru atalipa Sh milioni tano.
“Sio wanyama wote bali ni kwa kuanzia tumeanza na faru. Hata hivyo mtu akipenda aina fulani ya mnyama mfano akampenda fisi na kutaka kumpa jina lake tunaweza kumpa jina na hata kumuasili.”alisema Mwakilema.
Alisema pia kuna programu ya kuasili faru na ukitaka kumuona kila mwaka unachangia Sh milioni 1 ikiwa ni gharama za kumtunza.
Mkurugenzi Mtendaji wa TTB, Damas Mfugale ameipongeza Tanapa kwa ubunifu huo kwa kuwa utaongeza mapato kwa sababu watu wanavutiwa na wanyama.
Alisema kama Tanapa kuna mawazo tofauti ya namna ya kufanya kuingiza kipato ifanye lakini isipoteze maana ya uhifadhi.
“Isije tena kuelemea sana kwenye biashara ikasahau maana ya uhifadhi unajua Tanzania ni kitivo cha utalii hivyo ni lazima tuhakikishe kila tunachofanya tuendelee kuwa na vivutio bora ili tupate watalii,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Tato, Cyrill Ako alisema uamuzi wa Tanapa utapunguza ujangili.
Mpango huo wa Tanapa umekuja baada ya kuwepo kwa wanyama waliopewa majina kama faru John, faru Rajabu na Simba aliyefahamika kwa jina la Bob Juniour.
Kwa mujibu wa Mwakilema Bob Juniour aliyekufa Machi mwaka huu kwenye Hifadhi ya Taifa Serengeti alipewa jina hilo na waongoza utalii baada ya kulinganisha mnyama huyo na msanii wa muziki wa Raggae kutoka Jamaica Bob Marley.
Faru Rajabu alikufa Machi mwaka jana kwenye hifadhi ya Serengeti akiwa na umri wa miaka 43.
Mnyama huyo alikuwa mtoto wa faru John aliyekufa mwaka 2015 akiwa na umri wa miaka 47.