Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TanTrade yazindua Lebo ya Viungo Tanzania

E3de3aeae425b0d5b7bd6a4b893024fb.jpeg TanTrade yazindua Lebo ya Viungo Tanzania

Sat, 10 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KATIKA kutekeleza kwa vitendo ndoto za Rais Samia Suluhu Hassan kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji na wafanyabiashara nchini, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Dar es Salaam ( TanTrade) kwa kushirikiana na taasisi za sekta binafsi, imezindua Lebo ya Viungo Tanzania.

Lebo hiyo inalenga kuongeza thamani ya bidhaa za viungo vya Tanzania kimataifa na kwamba Wizara ya Viwanda na Biashara imeiagiza TanTrade kuwatambua wadau wote wa sekta ya viungo wakiwamo wakulima na wajasiriamali, kuwafikisha katika kilele cha juu ya biashara hiyo duniani.

Akizindua lebo hiyo jana katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF), Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, alisema ni hatua mojawapo ya kutafsiri kwa vitendo ndoto za Rais Samia kuhakikisha bidhaa za Tanzania zinaenea duniani kote.

"Kama mnakumbuka, Juni 26 katika Mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara, Rais Samia alieleza nia ya serikali yake ya awamu ya sita kuifanya nchi na fursa zake zote kujulikana duniani kote. Agizo hilo sisi ni watekelezaji na tumeanza na haya," alisema Kigahe.

Akifafanua kuwa, uzinduzi wa lebo hiyo unaongeza ubora na thamani ya viungo vya Tanzania ambavyo sasa vipo zaidi ya aina 30 sokoni na hasa kuongeza thamani ya viungo aina tano vya kimkakati ambavyo ni karafuu, pilipili manga, mdalasini, tangawizi na iliki yenye soko kubwa kimataifa.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dotto James, aliwahakikishia wadau wa sekta ya viungo nchini kuwa serikali utawashika mkono kuwafikisha wanakotaka.

Mwenyekiti wa Wazalishaji wa Viungo (TASPA) na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Lebo ya Viungo Tanzania (TSL SC), Edward Rukaka, alisema jambo hilo walilisubiri muda mrefu na kuishukuru serikali kuwawezesha kuongeza ubora wa bidhaa, kuzitambulisha na kushiriki katika ushindani wa soko.

Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Edwin Rutagerura, alisema lebo hiyo itatofautisha bidhaa za viungo za Tanzania na nchi nyingine na kumaliza tabia ya wafanyabiashara kutumia nembo zao kujimilikisha na kuuza bidhaa hizo za Tanzania. "Cha msingi tuzingatie ubora, tusichanganye mbegu za papai na pilipili manga, tuzingatie ubora,"Alisisitiza.

Mshauri Mkuu wa Lebo ya Viungo Tanzania, Profesa Amon Maerere, alisema lebo hiyo imeandaliwa kwa mwaka mmoja na nusu na walipokea maoni ya wadau wakubwa wa viungo zikiwamo nchi za Uingereza, Ujerumami na Ufaransa na kudhihirisha Tanzania ina ina uwezo mkubwa wa kuzalisha viungo tangu miaka ya 1880.

Chanzo: www.habarileo.co.tz