Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TanGreen kuzalisha tani 10,000 za samaki

SAMAKI TanGreen kuzalisha tani 10,000 za samaki

Tue, 28 Sep 2021 Chanzo: mwananchidigital

Kampuni ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ya TanGreen inatarajia kuzalisha tani 10,000 za samaki kwa mwaka ifikapo mwaka 2022 ili kupunguza usafirishaji wa samaki kutoka nje ya nchi.

Kampuni hiyo iliyoanza ufugaji wa samaki na uzalishaji wa vifaranga wa samaki mwaka 2019 katika kijiji cha Kigangama kata ya Kigongosima wilayani Magu mkoani Mwanza imesema mpaka sasa imeshawekeza Sh2.6 bilioni katika ufugaji huo katika eneo lenye ukubwa wa ekari 55 ili kupunguza utegemezi wa rasilimali hiyo kutoka ziwani.

Daktari wa samaki na ufugaji wa samaki kwa njia ya mabwawa wa kampuni hiyo, Dk Mugure Mariwanda amesema hadi sasa vifaranga 1,000,000 vimeshazalishwa katika vizimba 24 vilivyoko katika eneo hilo.

"Malengo yetu ni kufikisha vizimba 1,200 vya kukuzia vifaranga na kuongeza mabwawa ya kufugia samaki kutoka 17 hadi 34 ili kuongeza uzalishaji wa sato na kupunguza utegemezi wa ziwa Victoria katika kutoa kitoweo cha sato kwa ajili ya matumizi na viwandani," amesema Mariwanda.

Akizungumza alipotembelea mradi huo naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na mahitaji ya vifaranga vya samaki zaidi ya milioni 42 huku uzalishaji wa sasa ukiwa ni vifaranga milioni 22 pekee.

"Kwa upande wa vyakula vya samaki mahitaji ni yanakadiriwa kuwa ni tani 9,552 huku uwezo wa viwanda vyetu ni kuzalisha tani 875 tu," amesema Ulega.

Ulega amesema ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji na ufugaji wa samaki hao, Serikali imeruhusu wafanyabiashara kuingiza vifaranga vya samaki kutoka nje ya nchi na kuondoa baadhi ya tozo ikiwemo tozo ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye bidhaa za uzalishaji na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ili kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji katika sekta hiyo nchini.

"Niwaombe wafanyabiashara na wananchi kujitokeza kwa wingi kuwekeza katika uchumi huu wa bluu, kuna fursa nyingi serikali itazidi kuweka mazingira wezeshi ili kuwasaidia kuzalisha samaki kwa njia hii mbadala ambayo ni rafiki na isiyo athiri mazingira ya ziwa na bahari."

"Ufugaji huo wa kutumia vizimba ni rafiki kwa mazingira lakini pia unasaidia kupunguza uingizwaji wa kitoweo hicho kutoka nje ya nchi," amesema Ulega.

Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kali amesema wilaya hiyo bado ina maeneo ya kutosha kwa ajili ya wawekezaji katika ufugaji kwa kutumia vizimba huku akiahidi kwa walio tayari kuwekeza wilayani humo milango ya ofisi yake ipo wazi.

Chanzo: mwananchidigital