Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tamstoa yataka suluhu ushushaji bei ya mafuta

Waagizaji Mafuta Wakanusha Upotoshaji Unaosambazwa Mitandaoni.jpeg Tamstoa yataka suluhu ushushaji bei ya mafuta

Fri, 8 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha Wamiliki wa Malori wa Kati na Wadogo nchini (Tamstoa), kimeitaka Serikali kuja na mwarobaini wa kushusha bei ya mafuta badala ya kujikita zaidi kwenye kutafuta ufumbuzi wa upatikanaji wake.

Kauli hiyo ya Tamstoa inakuja ikiwa imepita saa chache tangu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kumpa siku saba Naibu Waziri Mkuu, Dotto Biteko, kukaa na wadau wa mafuta ili washughulikie changamoto ya upatikanaji wa bidhaa hiyo.

Hii ni baada ya kuwepo kwa tabu ya upatikanaji wake katika baadhi ya maeneo nchini.

Akizungumza leo Alhamisi Septemba 7, 2023 na waandishi wa habari Mwenyekiti wa Tamstoa, Chuki Shabani, amesema Serikali katika sakata hilo inapaswa kuangalia zaidi namna ya kushusha bei kwa kuwa tatizo hilo ni kubwa kuliko hata upatikanaji wake.

Septemba 4 mwaka huu, Mamlaka ya Udhibiti wa Hudima za Nishati na Maji (Ewura), ilitangaza bei mpya ya mafuta na kwa jiji la Dar es Salam, petroli inauzwa Sh3213, huku dizeli ikiuzwa Sh3259, bei ambazo zimepaa ikilinganishwa na zile za mwezi Agosti.

Katika tamko hilo, mwenyekeiti huyo amesema inasikitisha kuona Zambia ambao wanachukulia mafuta hapa nchini bei yao ya mafuta ni sawa na Sh999.

Kama haitoshi visiwani Zanzibar nako bei ya mafuta ipo chini kwani mpaka kufika jana yalikuwa yakiuzwa Sh2893 na kuhoji Serikali inakwama wapi kutafuta suluhu ya kupunguza bei ya bidhaa hiyo ambayo haiwaathiri tu wao bali na wananchi wakawaida.

"Leo hii wasafirishaji hatujui bajeti ya kusafirisha mzigo kwa sababu kila leo mafuta yanapanda na haujui yatapanda kwa shilingi ngapi.

"Kwa kweli inatuumiza ukizingatia wengi wanapenda kuweka mafuta yao nchini hata kama wanasafiri kwenda nje ya nchi ili kuhakikisha wanaacha hela hapa ili ziwanifaishe watanzania na sio kuwapelekea nchi nyingine," amesema Shabani.

Katika ushauri wake amewataka mawaziri wanaohusika na nishati kuangalia namna ya kupata ruzuku ya mafuta kwa wazalishaji wakubwa duniani kwa kuhangaika kuwafikia kama anavyofanya Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kuhangaikia mbolea ya ruzuku ambayo sasa upatikanaji wake huwezi kuulinganisha na kipindi cha nyuma.

Pia ameishauri Serikali kuwa na hifadhi yake ya mafuta ili yanapokuwa adimu, wanayaachia sokoni kudhibiti hali hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live