Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Takukuru kuvalia njuga utapeli, wanaoghushi risiti za EFD

Efdpic Data Takukuru kuvalia njuga utapeli, wanaoghushi risiti za EFD

Thu, 8 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Shinyanga imeanza kuchukua hatua kwa kuchunguza watu wanaotapeli wananchi kwa kuwapigia simu wakidai wao ni maofisa wa taasisi hiyo kisha kuwataka wawapatie fedha.

Akitoa taarifa ya kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023/2024 leo Februari 7, 2024 kwa waandishi wa habari, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy amesema kuna watu wanawapigia simu wadau mbalimbali na kujifanya ni maofisa wa Takukuru na wamepata tatizo, hivyo kuwaomba wawatumie fedha.

Amesema kitendo hicho ni utapeli na tayari wameanza kuchukua hatua ili kuwabaini.

Amewatahadharisha wananchi kuwa makini na watu hao, ambao wana nia ya kuwatapeli, akisisitiza utoaji wa taarifa.

“Tumekuwa tukipewa taarifa na sasa tumechukua hatua ya kufanya uchunguzi ili kuwabaini,” amesema.

Katika hatua nyingine, amesema wamebaini uwepo wa risiti za mashine za EFD za kughushi zinazotolewa na baadhi ya wazabuni wanaofanya biashara kwenye halmashauri.

Mambo mengine waliyobaini ni uwepo wa EFD zenye namba ya utambulisho wa mfanyabiashara tofauti na anayetoa huduma au bidhaa.

Kutokana na changamoto hiyo, wameshauri elimu iendelee kutolewa kwa wananchi ili wajue matumizi sahihi ya mashine za EFD.

Amesema jumla ya miradi 13 ya maendeleo yenye thamani ya Sh5.2 bilioni imefikiwa na Takukuru kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na kubaini haina mapungufu.

Akizungumzia hilo, Ramadhan Juma, mkazi wa Manispaa ya Shinyanga amesema kugushi risiti za EFD kunatokana na wafanyabiashara kulindana, jambo ambalo limekuwa likisababisha kuendeleza vitendo vya rushwa.

Maige Clement, mkazi wa Ngokolo ameiomba Serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria wanaoghushi risiti za EFD kwa kuwa wanahujumu uchumi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live