Taka za chupa za kioo na karatasi zimeweza kuboreshwa na kutengenezwa mapambo ya ndani.
Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Kadaso Kipingili amesema hayo alipozungumza na HabariLEO kuhusu uchakataji wa taka ngumu hizo.
Amesema wamefanya utafiti wa kuchakata chupa za kioo kwa kuziponda ponda, kulainisha kisha kuzalisha shanga kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya mapambo.
“Tunafanya hivi kwa sababu shanga zote zinatokana na chupa baada ya kupata shanga hizo tunazitumia pia kuremba chupa hizo ambazo pia tumeziokota.
“Chupa yenyewe inazalisha shanga na chupa zenyewe zinarembwa kuwa pambo ambalo litatumika nyumbani. Katika karatasi tunachana, tunaloeka kwenye maji tunalaainisha kisha tunatwanga,” amesema.
Amesema kwa kuponda karatasi unapatikana udongo ambao unafinyangia vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuuweka rangi mbalimbali.
“Vitu hivi tumevichagua kwa sababu kwa sasa vinachafua sana mazingira na vinapoteza baadhi ya viumbe ambao wanaendelea na maisha yao.
“Sisi tumetumia shanga kurudisha kwenye chupa na kuboresha chupa zetu na sasa zimeongezeka thamani,” amesema.