SERIKALI imewataka wananchi kuepuka kuingiza gesi nchini zilizopigwa marufuku na vifaa vinavyotumia gesi haribifu ikiwamo majokofu na viyoyozi vya mitumba ili kulinda tabaka la Ozoni.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, alibainisha hayo jana jijini hapa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni.
“Septemba 16, mwaka huu, tutaungana na jumuiya ya kimataifa kuadhimisha siku ya kimataifa ya hifadhi ya tabaka la Ozoni kama ilivyoagizwa na makutano mkuu wa Umoja wa Mataifa katika azimio lake namba 49/114 la tarehe 19, Desemba 1998,” alisema Jafo.
Jafo alisema, tabaka la Ozoni linapoharibiwa huchangia kuruhusu mionzi zaidi kufika kwenye uso wa dunia na hivyo kusababisha kuongezeka kwa magonjwa kama vile saratani ya ngozi, uharibifu wa macho yaani mtoto wa jicho unaosababisha upofu.
“Pia husababisha upungufu wa kinga dhidi ya maradhi na kujikunja kwa ngozi,” alisema Jafo.
Kadhalika, alisema madhara mengine ni kuharibika mimea hasa mazao ya kilimo kutokana na kuathirika kwa maumbile na mifumo ya ukuaji.
“Vilevile baadhi ya kemikali hizi husababisha kuongezeka kwa joto duniani na hivyo kuchangia katika mabadiliko ya tabianchi,” alisisitiza waziri huyo.
Alisema ili kulinda tabaka hilo serikali za mataifa mbalimbali zilikubaliana kuunda mkataba wa Viena wa hifadhi ya tabaka la Ozoni mwaka 1985.
“Mkataba huu unasisitiza ushirikiano katika utafiti usimamizi na ubadilishanaji wa taarifa za hali za tabaka la Ozoni kutokana na kupungua kwa matumizi yake,” alisema.
Alisema pia ilianzishwa Itifaki ya Montreal inayohusu udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa tabaka la Ozoni.
Alisema ili kudhibiti hali hiyo serikali pia inasisitiza kuingiza nchini vipoozi mbadala na rafiki kwa tabaka la Ozoni kama vile R209, R407, R404 na R717.
“Pia kununua bidhaa zilizowekwa nembo rasmi isemayo ‘Ozone friendly’ yaani Sahibu wa Ozoni au CFC-free ikiashiria haina wala haikutengenezwa na kemikali zinazomong’onyoa tabaka la Ozoni,” alisema.
Jafo, alisema wananchi wanatakiwa kuepuka kutupa ovyo majokofu ya zamani ama vifaa vya kuzimia moto vyenye kemikali zinazomong’onyoa tabaka la Ozoni aina ya CFCs na halon.