Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tafiti ndizo zitanyanyua zaidi kilimo

23f77ac872ce0733ef0e15b2ad462543 Tafiti ndizo zitanyanyua zaidi kilimo

Tue, 1 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ENDAPO watafiti na wadau mbalimbali wa kilimo nchini watajikita vyema katika matumizi ya sayansi na teknolojia pamoja na kufanya tafiti zenye ubora katika kilimo, nchi za Afrika zitapiga hatua kubwa katika kuzalisha mazao ya kilimo na kuongeza kipato.

Hayo yanasemwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Selian mkoani Arusha, Dk Joseph Ndunguru, wakati akiwasilisha mada katika Jukwaa la Kuunganisha Watafiti na wadau mbalimbali wa kilimo lililofanyika hivi karibuni jijini Arusha.

Katika mada yake iliyoangalia mchango wa watafiti katika kuleta mageuzi ya kilimo, Dk Ndunguru anasema kwa kuwa asilimia 60 ya ardhi inayofaa kwa kilimo duniani ipo Afrika, watafiti wa Afrika wana dhima kubwa ya kuhakikisha bara hilo linaongoza katika uzalishaji wa mazao.

Anasema kwa Tanzania mchango wa kilimo katika pato la taifa ni wastani wa asilimia 15, kiasi anachosema bado ni kidogo na kinamaanisha kwamba kuna shida kwenye tija na uongezaji wa thamani.

“Kuongeza tija ndio jambo kubwa. Ukiangalia mpango wa ASDP II kwenye eneo la kwanza la matumizi ya maji, udongo, tija na ongezeko la thamani, ili yote yaweze kufanyika matumizi ya tafiti ni muhimu sana. Hii ni pamoja kuangalia namna gani utafiti utatutoa tulipo sasa,” anasema.

Dk Ndunguru anakumbusha kwamba mkakati wa Tanzania katika kuelekea uchumi wa viwanda unaaminisha kwamba sehemu kubwa ya malighafi zitazohitajika zitatoka kwenye sekta ya kilimo.

Kwa mantiki hiyo anasema watafiti wategemee kuona mageuzi yakitakiwa kufanyika katika kilimo na kwamba Tanzania inabidi kuongeza kipaumbele katika suala zima la utafiti.

“Ni namna gani tafiti zitachangia kuleta mageuzi ya kilimo, kuongeza tija na kutatua changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi? Tukiwa na utafiti ambao unahusisha matumizi ya sayansi na teknolojia tunaweza kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao.

“Tutaweza pia kueleza wapi tulime zao lipi na kutumia mbolea gani,” anasema Dk Ndunguru.

Anasema matumizi ya sayansi yanayohusisha vipimo vya vinasaba (DNA) yanatakiwa kuongezeka kwa kuwa yanasaidia kuonesha kwamba hata wadudu wanaofanana kwa macho, wakipimwa wanaweza kugundulika kuwa ni jamii tofauti na kwamba kila koo ya wadudu hao inaweza kudhibitiwa na viuatilifu tofauti na kingine.

“Hii teknolojia ya kipimo cha DNA ipo Tanzania, tupime udongo, tuachane na kipimo cha zamani ili tufanye uamuzi sahihi wa udongo upi unafaa kwa kulima zao gani.

“Vile vile tujikite zaidi katika matumizi ya sayansi katika kuharakisha ugunduzi wa mbegu badala ya kufuata mlolongo wa kawaida,” anasema na kuongeza kwamba kupitia utafiti matokeo chanya ya maendeleo ya kilimo nchini yanaweza kupatikana.

Anasema ingawa tafiti nyingi zimefanyika nchini, wakati mwingine zilikuwa hazileti matokeo chanya na kwamba tatizo sio tafiti hizo bali ni namna gani zinavyofikishwa kwa walengwa na wadau wengine.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TARI taifa, Dk Geofrey Mkamilo, anasema lengo la kuwakutanisha wadau wa utafiti na sekta ya mbegu nchini ni kuangalia changamoto zinazowakabili wakulima ikiwemo matumizi hafifu ya pembejeo.

Anasema jukwaa hilo ambalo mada kuu ilihusu ‘Teknolojia za Kilimo na Uvumbuzi kwa Maendeleo ya Uchumi’, lililenga kupata majibu yatakayotoa matokeo chanya ili wananchi waweze kulima kilimo chenye tija na siyo cha kujikimu.

Anaeleza kuwa hata tafiti mbalimbali zinazoendelea kupelekwa kwa wakulima inaonekana matumizi yake ni madogo. Dk Mkamilo pia anawataka watafiti kuangalia eneo la zana za bora na rahisi za kilimo ili kuwakomboa wakulima na jembe la mkono.

“Umaskini wetu utaendelea kwa sababu ya kutumia jembe la mkono hata tukiwa na mbegu bora na matumizi ya mbolea. Tukiendelea na jembe la mkono mabadiliko tunayoyataka katika kilimo yatachelewa sana. Lazima teknolojia hiyo ibadilike,” anasema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TARI, Dk Yohana Budeba, anashukuru hatua ya watafiti kukutana na wazalishaji wa makampuni ya mbegu kwa kila mwaka ili kujadili mikakati mbalimbali ya kuboresha uzalishaji wa mbegu, usambazaji wake na matumizi ya mbegu bora ambazo watafiti wanazigundua.

Anaishukuru TARI kwa kugundua mbegu bora pamoja na kuendeleza teknolojia mbalimbali za kuboresha kilimo.

Anaweka msisitizo kuwa matokeo ya tafiti na matumizi ya teknolojia mbalimbali zilizogunduliwa ni vyema zisibaki kwenye makabrasha bali ziwafikie wakulima ili walime kilimo chenye tija.

Anasema maazimio mbalimbali yaliyopatikana katika mkutano huo yatasaidia serikali katika kutunga sera zake na sheria mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya kilimo nchini.

Anasema kilimo cha Tanzania bado kina tija ndogo kutokana na kutegemea mvua, huku pia kikikabiliwa na changamoto za visumbufu vya mazao; wadudu na magonjwa. Ni kwa mantiki hiyo anazidi kuishauri serikali kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya tafiti ili kuwawezesha wakulima kuongeza tija katika kuzalisha mazao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu kutoka TARI, Makao Makuu jijini Dodoma, Eveline Lukonde, anasema taasisi hiyo ipo kwa ajili ya utafiti wa mbegu bora sambamba na kugundua teknolojia za kilimo bora katika kupambana na wadudu na magonjwa ya mazao.

Anasema pia wanaangalia masuala ya udongo kwani ni kitu muhimu sana katika kuboresha uzalishaji. Anafafanua kwamba unaweza kupata mazao ya kutosha au kupoteza kabisa kama udongo husika utakuwa hauna afya kwa zao husika.

Anasema mafanikio waliyoyapata kwa miaka miwili tangu kuanzishwa kwa TARI ni pamoja na kugundua zaidi ya mbegu bora 148 za mazao mbalimbali huku nyingine 26 zikisubiri kwenda kwa wakulima.

Anasema wameandaa ramani mbili muhimu ikiwemo ya udongo inayoonesha maeneo yenye udongo wenye tindikali katika mikoa 18.

“Tumeweza kugundua teknolojia 36 katika uongezaji wa thamani na usindikaji, pia teknolojia 20 katika masuala ya kilimo bora katika mazao mbalimbali,” anasema.

Anasema bado kuna changamoto wanazokutana nazo, ikiwemo miundombinu upande wa maabara kwa kuwa nyingi hazina sifa ya kimataifa.

Anasema kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ukame ni tatizo kubwa na hivyo watafiti wa TARI wanahitaji kuwa na maeneo ya umwagiliaji.

Chanzo: habarileo.co.tz