Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tafiri kufanya tafiti sekta ya uvuvi

Uvuvi Haramu Tafiri kufanya tafiti sekta ya uvuvi

Tue, 10 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ikishirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) pamoja na Chuo Kikuu Cha DUKE cha nchini Marekani inafanya tafiti ya kufahamu na kupata taarifa sahihi ya rasilimali za uvuvi zilizopo hapa nchini ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika pato la taifa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa warsha inayoangalia mchango wa tafiti katika sekta ya uvuvi; Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Lukanga amesema tafiti hizo zitaibua taarifa za maeneo ambayo sehemu ya maziwa na Bahari ya Hindi iliyopo nchini kuweka taarifa zake sahihi kulingana na idadi ya watu ambao wamekuwa wakinufaika kupitia rasilimali zilizopo katika maji hayo.

Bw. Lukanga ameongeza kuwa kwa sasa idadi ya watu nchini imeongezeka na kufikia zaidi ya milioni sitini ila bado taarifa zilizopo kwenye sekta ya uvuvi zinatolewa kulingana na idadi ya watu iliyokuwepo zamani ya zaidi ya milioni 40 ambayo imekuwa ikibainisha watu wanaojishughulisha moja kwa moja katika sekta ya uvuvi ni milioni nne na nusu.

Aidha, amesema warsha hiyo imeanzishwa na wanasayansi na watafiti kutoka nchi zaidi ya 58 kuhakikisha rasilimali ambazo hazijionyeshi kwa uwazi ziweze kuonekana hususan kwenye uvuvi mdogo ili kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la taifa.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utafiti pamoja na Uratibu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Mary Kishe amesema taasisi hiyo ambayo mwaka huu inafikisha miaka 40 imekuwa ikikusanya na kutafiti masuala mbalimbali ya sekta ya uvuvi lakini bado haijaangalia mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa na mtu mmoja mmoja.

Amesema kupitia warsha hiyo inayoendelea jijini Dar es Salaam, ambapo TAFIRI inashirikiana na FAO pamoja na Chuo Kikuu Cha DUKE cha nchini Marekani, wataweza kuunganisha taarifa za zamani na kuziweka pamoja na kuona umuhimu wa takwimu hizo kwa maendeleo endelevu ya sekta ya uvuvi kwa kuwa kuna taarifa ambazo zimejificha ambazo hazionyeshi usahihi juu ya sekta hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live