Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taboa yanuia kupandisha nauli

Nauli Pic Data Taboa yanuia kupandisha nauli

Fri, 9 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati bei ya mafuta ya dizeli ikiongezeka mwezi huu, Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kimesema kwa hali inavyoendelea wataomba kupewa bei mpya za nauli za mabasi.

Katibu wa Taboa, Priscus John alisema jana kuwa, “tulitegemea bei inavyoshuka katika soko la dunia na huku itashuka, ila imekuwa ndivyo sivyo.”

Juzi, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ilitangaza bei mpya za mafuta, huku petroli ikionekana kushuka kwa Dar es Salaam na baadhi ya mikoa ikianza kuhisi maumivu ya ongezeko la bei.

Licha ya kuwekwa kwa ruzuku ya Sh83, Sh247 na Sh243 kwa lita kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, bado bei ya dizeli imeonekana kuongezeka kwenye maeneo hayo.

Kwa upande wa dizeli ya rejareja sasa itauzwa kwa Sh3,247 kutoka Sh3,052 iliyokuwapo Novemba mwaka huu kwa upande wa Dar es Salaam, huku wakazi wa Tanga wakinunua kwa Sh3,496 kutoka Sh3,249 na Mtwara kwa Sh3,512 kutoka Sh3,269.

John alisema hali inavyoendelea Taboa watalazimika kuomba nauli mpya ili kuendana na gharama za uendeshaji wanazotumia, “abiria mjiandae, vinginevyo magari yatatushinda tutayaegesha.” Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) akijibu kuhusu maamuzi ya Taboa, alisema anawakaribisha kupeleka maoni yao na taratibu zipo wazi.

“Namna ya kwanza ni wao kuleta maoni, sisi tutayapeleka kwa wadau, baadaye kwa Baraza la Watumiaji Usafiri (Latra CCC), baadaye tunakaa mezani tunapanga bei.”

Wakati bei ya dizeli ikiongezeka na petroli ikishuka, mjadala umeibuka juu ya mwenendo wa utoaji wa ruzuku ya bidhaa hiyo iliyopungua na mamlaka haijadhihirisha.

Mei mwaka huu Serikali iliweka ruzuku ya Sh100 bilioni kwa ajili ya kupunguza makali ya bei. Julai 2022, ruzuku ya Sh100 bilioni iliwekwa na Agosti mwaka huu ruzuku ilisalia Sh100 bilioni kabla ya kuanza kushuka hadi Sh65 bilioni Septemba na Sh59.58 bilioni Oktoba, huku Novemba na Desemba hazijatajwa kiasi.

Akizungumzia mwenendo huo na kutokuwekwa kwa ruzuku kwenye mafuta ya petroli, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo alisema lengo la ruzuku ni kupunguza makali ya kupanda kwa bei za mafuta.

“Hivyo inapotokea eneo moja bei ipo juu huku eneo lingine ipo chini inabidi kuweka usawa. Mafuta ya petroli yanayoingilia Bandari ya Dar es Salaam hayakuwekewa ruzuku kwa kuwa yameshuka kutoka bei za Novemba.

“Mikoa tisa inategemea mafuta yanayopitia Bandari ya Dar es Salaam, kasoro Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Lindi, Mtwara na Ruvuma.” Hata hivyo, kwa Dar es Salaam petroli itauzwa kwa Sh2,827 kutoka Sh2,886 ya Novemba mwaka huu, sawa na punguzo la Sh59.

Lakini kulingana na ukomo wa bei ya mafuta, petroli kwa Tanga imefikia Sh2,815 kutoka Sh2,806 na Mtwara wakinunua lita moja ya petroli kwa Sh2,825 kutoka Sh2,917.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live