Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taasisi zakumbushwa kuhifadhi taarifa NIDC

A52f79161467d20c8f46a322764925a3 Taasisi zakumbushwa kuhifadhi taarifa NIDC

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WIZARA ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imezihimiza taasisi za serikali kukitumia Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data (NIDC) kuhifadhi taarifa mbalimbali.

Imesema kituo hicho ni sehemu salama, kina miundombinu, mifumo ya Tehama ya kisasa, wataalamu wabobezi na nafasi ya kutosha kwa ajili ya kuhifadhi taarifa mbalimbali.

Taarifa iliyolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika wizara hiyo imeeleza kuwa, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile aliyasema hayo wakati alipotembelea NIDC jijini Dar es Salaam juzi.

Katika ziara hiyo, Ndugulile alifuatana na Naibu Waziri wake, Kundo Mathew, Katibu Mkuu, Dk Zainabu Chaula, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba na watendaji wa wizara hiyo.

Wakati akiwa katika kituo hicho, Dk Ndugulile alibaini kuwa ni taasisi 84 tu za serikali kati ya 149 zinazotumia NIDC kuhifadhi taarifa.

Alizitaka taasisi za serikali kuzingatia agizo la Rais John Magufuli alilolitoa alipotembelea kituo hicho kuzindua mfumo wa kielektroniki wa kukusanya mapato (Electronic Revenue Collection System - eRCS) mwaka 2017.

Mfumo huo umeiwezesha NIDC kuongeza makusanyo ya mapato kutoka Sh bilioni 1.4 mwaka 2019 na kufikia Sh bilioni 2.76 mwaka huu.

Kwa upande wake, Mathew aliipongeza NIDC kwa kutengeneza mifumo ya Tehama ambayo inaiwezesha serikali kuongeza makusanyo ya mapato na kurahisisha maisha kuendana na mahitaji ya wananchi.

Alisema mifumo hiyo imewezesha kununua tiketi za mabasi kwa njia ya mtandao, kuweka mafuta kwenye magari, kulipa kiingilio kwenye uwanja wa mpira wa Benjamin Mkapa, usafiri wa kivuko cha Kigamboni, usajili wa leseni Brela na maegesho ya magari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Dk Chaula aliwahimiza watendaji NIDC washirikiane na wataalamu wa wizara ili kuhakikisha serikali inaendelea kuwahudumia wananchi kwa kutumia Tehama kuokoa muda wa kutafuta huduma za serikali.

Meneja wa NIDC, Geofrey Mpangala alisema wateja wanaotumia kituo hicho wamepunguza gharama za uendeshaji na uwekezaji kwenye taasisi zao kwa kuwa hawajengi miundombinu na mifumo ya Tehama, wateja wanapata viwango vya juu vya data yenye kasi na uhakika wa usalama wa data zao na huduma zinatolewa kituoni hapo kwa saa 24.

Kindamba alimshukuru Dk Ndugulile kwa ziara yake akisema imeongeza ari ya utendaji kazi kwa wataalamu wa NIDC pamoja na kuongeza idadi ya wateja na mifumo ya Tehama kutokana na kurahisisha huduma kwa wananchi

Chanzo: habarileo.co.tz