Taasisi ya Alliance Bioversity & CIAT inayohusika na utafiti wa maharage yenye makao yake nchini Kenya imeibuka mshindi wa tuzo ya Chakula Afrika ikipewa zawadi ya Dola 100,000 (Zaidi ya Sh250 milioni).
Tuzo hizo huandaliwa na Jukwaa la Mifumo ya Chakula (AGRF) kila mwaka na mshindi hukabidhiwa tuzo hiyo pindi mkutano unapofanyika.
Taasisi iliyoshinda, ina matawi katika nchi 31 za Afrika na imeshafanya tafiti za mbegu zaidi 650 za maharage huku baadhi yake zikitajwa kuwa na madini ya zinki na chuma na zenye uwezo wa kustahamili mabadiliko ya tabia nchi.
Akizungumza, Rais Mstaafu wa awamu tano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Kamati ya tuzo ya Chakula Afrika, Jakaya Kikwete amesema mchakato huo ulihusisha washiriki 496 waliopendekezwa kutoka nchi 47 tangu kufunguliwa kwake Februari 17, 2023 Accra nchini Ghana.
Tuzo hizo huwatambua watu waliopendekezwa au taasisi inayofanya kazi nzuri ya kuendeleza kilimo na Chakula Barani Afrika ili iweze kupata tuzo hiyo.
"Baada ya mchakato wa wapendekezwa 496 ulifanyika mchakato mwingine na kupatikana watu 19 ikiwa ni baada ya kamati kukutana Agosti 4 na 5 mwaka huu jijini Dar es Salaam ndipo taasisi hii ikaibuka mshindi," amesema Kikwete.
Tuzo hiyo imetolewa katika mkutano wa kumtangaza mshinfi huyo uliofanyika katika Jukwaa la Mifumo ya Chakula (AGRF) linaloendelea jijini hapa.
Moja ya sababu iliyofanya shirika hilo kushinda ni tafiti za maendeleo ya mbegu za maharage kwa miaka waliyofanya kazi uliosaidia upatikanaji wa mbegu 650 za zao hilo.
"Kati ya mbegu hizo kuna zile ambazo huzaa sana na kumfanya mkulima kupata mazao mengi, nyingine huhimili mabadiliko ya tabia nchi hasa ya joto huku nyingine zikiwa na madini ya zinki na madini ya chuma," amesema Kikwete.
Akizungumzia tuzo hiyo, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Jean Claude Rubyogo amesema hiyo ni chachu kwao na itachochea kufanya tafiti zaidi huku akieleza kuwa wameamua kujikita katika utafiti wa maharage kwa sababu ya faida zilizopo ndani yake.
"Mbegu hizi tunazozalisha pia zimekuwa zikisambazwa kwa wakulima wa maeneo mbalimbali ambao tunafanya nao kazi, kwa Tanzania tunafanya kazi na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari)," amesema.
Tuzo hizo zinazotolewa kwa mwaka wa 18 sasa tangu kuanza kwake mwaka 2005 huku Tanzania ikiwahi kushinda mara moja pekee.