Naibu Kamishna wa TRA, Bw. Msafiri Mbibo ameitaka, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na Maafisa Forodha wa TRA pamoja na maafisa wa taasisi nyingine za Serikali kuhakikisha kuwa wanahamasisha matumizi sahihi ya kisheria katika Vituo vya Huduma kwa Pamoja Mpakani ili watu mbalimbali wanaopita kupata huduma za kikodi mipakani waweze kuhamasika kutumia njia sahihi badala ya njia zisizo rasmi za kimagendo.
Akiwa katika mpaka wa Mutukula unaounganisha nchi ya Tanzania na Uganda uliopo mkoani Kagera.Bwana Mbibo amesema kwamba, lengo la kutaka kuwepo kwa matumizi sahihi ya sheria hizo katika maeneo ya mipakani ni kuzuia watumiaji kuacha kutumia njia zisizo rasmi ambazo zinaweza kuathiri takwimu za kiuchumi, na kuhatarisha usalama wa nchi na pia uingizaji bidhaa mbazo hazina viwango ambazo zitaumiza walaji wa ndani na zinaweza kuharibu mahusiano baina ya Tanzania na nchi za jirani.
“Kuziingiza bidhaa ambazo hazina viwango nchini kwetu na kupeleka bidhaa ambazo hazina viwango kwa nchi ambazo ni majirani zetu kutaharibu mahusiano yetu ya kibiashara pindi wakigundua tunaingiza nchini mwao bidhaa za namna hiyo, hivyo lazima tusimamie vizuri sheria ili mambo haya yasitokee”, alisema Mbibo.
Mpaka wa Mutukula kwa sasa ufanisi wake unaoongezeka mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka wa fedha uliopita wa 2020/2021 ulipangiwa lengo la kukusanya shilingi bilioni 21 na umefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 24 ambapo hiyo ni sawa ufanisi wa utendaji wa asilimia 114 ikilinganishwa na mwaka wa fedha wa 2019/2021 malengo yalikua ni kukusanya shilingi bilioni 18 na zikakusanywa shilingi bilioni 20 na zaidi.