Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taa za uvuvi zapigwa ‘stop’

Taa Za Uvuvi.png Taa za uvuvi zapigwa ‘stop’

Sun, 26 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

JUMUIYA ya vyama vya wavuvi (FUO) mkoani hapa, imeiomba serikali kuzuia matumizi ya taa za kuvua dagaa zilizotengenezwa kienyeji, kwani zinahatarisha afya za walaji, uchafuzi ziwa Victoria pamoja na kuchochea uvuvi haramu.

‘’Uvuvi haramu ni kutokana na taa hizo kuwa na mwanga mkali kupita kiasi, kati ya Wati (watts) 15 hadi 30, takribani mara tatu hadi sita ya kiwango kilichoruhusiwa na serikali, ambacho ni wati tano hadi tisa, “Mkurugenzi wa FUO, Juvenary Matagili, amesema.

“Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI) iligundua wati zinazofaa kwa uvuvi wa dagaa, lakini wavuvi wanakaidi. Mwanga wa taa za kienyeji ni mkali kiasi cha kuvuta hata sangara watoto waliopo umbali mrefu kutoka ilipo mitego ya dagaa, ambao pia huvuliwa wakati bado hawajatimiza umri,” alisema na kuongeza:

“Hata dagaa watoto nao huvuliwa , hatua ambayo inasababisha kupungua kwa mazao ya ziwa Victoria.”

Kwa upande wa afya za walaji, Matagili amesema: “ Ziko hatarini kwa sababu wakati wa uvuvi taa hizo hufungwa pembezoni mwa mitumbwi, zinalowana kwa kupigwa na mawimbi na kisha betri zake kuvujisha majimaji.”

Na wakati wa kusafirisha dagaa kwenda nchi kavu, taa huwekwa juu yake (dagaa), huku majimaji ya betri yakichuruzikia kitoweo hicho.

“Hii ni hatari kwa sababu tunaamini mchuzi wa betri unaotiririkia dagaa ni sumu, na wachuuzi pale mialoni wakinunua dagaa hawawasafishi ipasavyo kabla ya kuwakaanga. Serikali itupie jicho suala hili,” amesistiza.

Kuhusu uchafuzi mazingira, Mkurugenzi amesema mara nyingi taa hizo zilizotengenezwa kwa miti na maplastiki zikipigwa na maji zinakua hazifai tena kwa matumizi, hivyo wavuvi kuzitupa ziwani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live