Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TaFF yatoa  bilioni 2/- ruzuku ujenzi wa viwanda

1e93a6d4f5c04ae2387343ec115410f2 TaFF yatoa  bilioni 2/- ruzuku ujenzi wa viwanda

Tue, 16 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MFUKO wa Misitu Tanzania (TaFF) umetoa ruzuku ya Sh bilioni mbili katika miradi ya uhifadhi wa misitu na ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya asali kwa mwaka 2020-2021.

Akizungumza na wanahabari katika maonyesho ya nne ya Mifuko ya Programu ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi jijini Arusha, Katibu Talawa wa Mfuko wa Misitu Tanzania, Dk Tuli Msuya amesema katikaa kipindi cha mwaka 2020 - 2021, Mfuko ulitenga bajeti kiasi hicho cha Shbilioni mbili kwa ajili ya kutoa ruzuku.

Dk Tuli alisema kiasi hicho cha fedha za ruzuku zimegawanywa mara mbili; Ruzuku ya kawaida na ruzuku maalum inayotolewa kwa Taasisi za Serikali.

“Sisi katika ruzuku hii maalum tunahusika zaidi katika kugharamia ujenzi na uboreshaji wa viwanda vinne (4) vya kuchakata na kufungasha mazao ya nyuki katika wilaya ya Sikonge (Tabora), Bukombe (Geita), Kibondo (Kigoma), na Mlele (Katavi).”

Dk Tuli alisema kwa maana hiyo tumeanza na viwanda vinne vya kuchakata asali hivyo tunaposema ruzuku ya bilioni mbili utakuta zaidi ya bilioni mmoja inakwenda kuwezesha hivyo viwanda, inayobaki ndio wengine wanashindania katika miradi ya uhifadhi wa misitu na ufugaji nyuki.

“Tulianza na kutoa ruzuku kwa miradi isiyozidi 50, lakini hadi sasa tumetoa ruzuku katika miradi 587 kwenye mikoa 26 ya Tanzania Bara, hivyo mfuko unakua vizuri.”

Hata hivyo Dk Tuli alisema pamoja na kutoa kiasi hicho cha ruzuku bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo uhaba wa fedha pamoja na uelewa mdogo wa Wananchi.

“Tunapokea maandiko mengi kuliko uwezo wa fedha ambayo imetengwa kutoa ruzuku, wakati mwingine unaweza kukuta mtu amekidhi vigezo vya kupewa ruzuku, lakini fedha uliyotenga haitoshi kwahiyo tunalazimika kuweka vigezo vingine vya juu kidogo.

Aliongeza kusema changamoto nyingine ni watanzania wanaposikia tunakupa ruzuku au fedha wanaanza kufikiria mambo mengine kinyume na malengo ya mradi wake.

“Baadhi ya wadau wanatumia hizi fedha kinyume na shughuli iliyokusudiwa, kwa hiyo tunalazimika kufuata sheria ili kukuhakikisha zile shughuli zilizokusudiwa zinatekelezwa au fedha ya serikali inarudishwa,” alisema Katibu Tawala wa TaFF.

Katika tangazo la mwaka huu la kuitisha maandiko ya ruzuku, makampuni na watu binafsi wanashauriwa kutowasilisha maombi kwa kuwa hayatafikiriwa.

“Watu binafsi wasijisumbue kuomba ruzuku mwaka huu kwa sababu watakuwa wamepoteza muda wao, labda tutakapopata fedha za kutosha kwa wakati mwingine tutaweza kuwafikiria au kutengeneza utaratibu mwingine,” alisema Dk Tuli.

Aliongeza kusema katika tathimini iliyofanyika kwa nini watu binafsi hawajapewa kipaumbele cha kupewa ruzuku, kimsingi watu binafsi na makampuni mengi yenye sura ya watu binafsi ni vigumu sana kufuatilia hasa wanapoambiwa ni ruzuku.

“Mfano unaweza kumpa mtu ruzuku leo yupo kijiji hichi, kesho unamkuta mtu amehama kabisa kijijini kwa hiyo tunaanza kusumbuana kumtafuta, lakini kama ni kikundi hata akiondoka mtu mmoja wadau wengine wataendelea kuwepo.”

Katibu Tawala wa TaFF, Dk Tuli alisema watu binafsi unaandaliwa utaratibu mzuri ambao utahakikisha fedha ya Serikali ikitolewa inaweza kufuatiliwa wakati wa kutimiza malengo ya miradi.

Chanzo: habarileo.co.tz