Taasisi ya utafiti wa kahawa nchini (TaCRI) imeanza kusambaza bidhaa kupitia mradi wake wa ongezeko la mnyonyoro wa thamani.
Lengo la usambazaji huo ni kuhamasisha wakulima, kuongeza thamani ya kahawa ili kufanikisha jitihada za kuboresha maisha ya wakulima kupitia kilimo cha zao hilo.
Mkurugenzi mkuu mtendaji wa TaCRI, Dk Deusdedity Kilambo ameyasema hayo leo Jumamosi Oktoba 30,2021 wakati akizungumza na wauzaji wa kahawa katika vijiwe mbalimbali vya kahawa mjini Moshi alipowatembelea na kusambaza bidhaa hiyo.
Dk Kilambo amesema wanatumia bidhaa wanayozizalisha kuelekeza wakulima namna ya kuiongezea thamani kahawa, hatua ambayo itawawezesha kuiuza kwa bei ya juu zaidi ya ile ghafi na kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo cha zao hilo.
“Leo tumezungukia vijiwe mbalimbali vya kahawa mjini Moshi lengo letu ni kuendelea kuthibitisha ubora wa tafiti zetu, kwa sababu tumetoa aina mpya ambazo zinasifa za ukinzani kwenye magonjwa lakini pia ina ladha na muonjo mzuri, kwa hiyo tumesambaza sampuli za bidhaa yetu tunayozalisha, ili kuendelea kuthibitisha ubora wa kahawa na tafiti zetu."
“Lakini kusambaza bidhaa hii pia ni kuwaelekeza wakulima namna ya kufanya ubora wa ongezeko la thamani uwezekane, kwa sababu wakulima wetu wengi wa kahawa, wamezoea kuuza kahawa katika daraja la Pachment, sasa tunawahamasisha waiongezee thamani, ili waweze kupata bei nzuri zaidi," amesema.
Wakizungumza baadhi ya wauzaji wa kahawa, katika vijiwe vya kahawa mjini Moshi, mbali na kusifia kahawa hiyo kuwa bora, waliomba bei ipunguzwe ili kuweza kumudu gharama na kufanikisha jitihada zao za kujiongezea kipato na kujikwamua kiuchumi..
“Kahawa hii ni nzuri na namna ninavyoitengeneza, wateja wangu wanaisifia sana, lakini tatizo ni bei tunayouziwa, pakti ya gramu 100 tunauziwa Sh 2,000, lakini tukitaka kilo moja ni Sh 20,000, tunaomba tupunguziwe bei kidogo, ili tunapofanya biashara ya kinywaji cha kahawa, na sisi tuweze kupata faida nzuri," amesema Shaban Seleman.