Dar es Salaam. Mwenyekiti wa bodi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Omary Nundu amesema shirika hilo linahitaji Sh1.77trilioni kuboresha huduma zake za simu za mkononi na mezani.
Fedha hizo zitatumika kukamilisha mipango ya shirika hilo ya kutaka kuongeza kima cha huduma zake sokoni walau kufika asilimia 15 kwa simu za kiganjani na kwa asilimia 98 katika simu za mezani.
Nundu ametoa kauli hiyo leo Jumanne Mei 21, 2019 katika hafla ya shirika hilo kutoa gawio kwa Serikal iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa awamu ya pili ya huduma ya video conference.
Mwenyekiti huyo wa bodi amesema kufanya hivyo kutalifanya shirika kupata faida kubwa jambo litakaloongeza gawio kwa Serikali.
“Uwekezaji huo ni kwa ajili ya kipindi cha miaka mitano kuanzia 2017/2018 lakini hadi hivi sasa tuko nyuma ya azma kwa miaka miwili na kadri tunavyochelewesha ndiyo inazidi kutuwia vigumu kufikia kwani washindani wetu wanazidi kujiimarisha na kuzidi kufika mbali,” amesema Nundu.
“Mahitaji haya yanagawanyika kwenye uwekezaji na huduma za kiganjani ni asilimia 67 ya fedha hiyo inayobakia ni kwa ajili ya huduma ya simu za mezani.”
Habari zinazohusiana na hii
- TTCL yatoa gawio la Sh2.1 bilioni kwa Serikali
- Nundu: Bila Magufuli TTCL ingekufa
- Sheikh Kipozeo: Magufuli I love you so much
Ameongeza, “Fedha hizi zikipatikana kwa wakati sio tu TTCL itaweza kukabiliana na ushindani wa kibiashara uliopo katika soko la huduma za mawasiliano lililopo nchini bali pia litaweza kufanya yenye tija katika teknolojia, mitambo na miundombinu, pia itakidhi jukumu lake la kusambaza huduma zake nchi nzima hasa vijijini.”
Amesema baada ya kupanuka wataweza kuanzisha viwanda, kutoa huduma ya fedha taslimu kupitia simu ya mkononi.