Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TTCL kuunganisha Mkongo wa Taifa Bara na Z’bar

C34ec8fa667d2b3ecc12b865ed71ef2c.png TTCL kuunganisha Mkongo wa Taifa Bara na Z’bar

Fri, 25 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limetia saini ya makubaliano ya kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na wa Zanzibar.

Tukio hilo lilishuhudiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dk Zainabu Chaula na Dk Mustafa Aboud Jumbe, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Zanzibar.

Makubaliano hayo yameingiwa rasmi kati ya TTCL kupitia Mkurugenzi Mkuu Waziri Kindamba na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Uendeshaji Mkongo Zanzibar (ZICTIA), Shukuru Awadh Suleiman.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL , Kindamba alisema taratibu zote muhimu za kitaalamu na kiufundi kwa pande zote mbili ya Tanzania Bara na Zanzibar zimekamilika ikiwa ni kufanikisha majaribio yaliyofanywa miezi kadhaa iliyopita ya kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Mkongo wa Zanzibar kupitia vituo vya Tanga - Pemba na Dar es Salaam - Unguja.

“Kufanikisha kuunganisha Mkongo Taifa na huu wa Zanzibar, ni fursa pekee kwa watoa huduma mbalimbali za kijamii, uwekezaji, kibiashara na kiuchumi kwa pande zote mbili kufikia masoko au wateja wao kwa urahisi, haraka zaidi na kwa gharama nafuu,”alisema Kindamba.

Mtendaji Mkuu wa ZICTIA, Suleiman alisema makubaliano hayo yanatokana na na ushirikiano mkubwa wa kiutendaji kati ya taasisi hizo mbili, na utaleta mageuzi makubwa katika matumizi ya mawasiliano pamoja na kukuza uchumi wa taifa.

Katibu Mkuu, Chaula alizitaka taasisi hizo mbili TTCL na ZICTIA kuhakikisha wanasimamia vyema na kulinda miundombinu hiyo ya mkongo ya mawasiliano ili huduma za mawasiliano zipatikane muda wote.

“Ni wazi kuwa uwepo wa Mkongo wa Zanzibar ambao umeunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unaenda kufungua fursa kwa wawekezaji na watoa huduma mbalimbali ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwa sababu kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano tumefanikisha kuunganisha nchi za Afrika Mashariki na kati ikiwemo Rwanda, Burundi, Kenya, Congo, Zambia, Malawi na Uganda,”alisema Chaula.

Alisema ufunguzi wa njia ya Mawasiliano ya Mkongo kati ya Tanzania Bara na Zanzibar utakuwa na manufaa makubwa kwa Taifa ambapo itaongeza kasi ya matumizi ya huduma za data na intaneti sambamba na huduma nyingine za kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Dk Mustafa Aboud Jumbe alisema Mkongo wa Zanzibar umefanikisha kuunganisha mikoa na wilaya zote za Ugunja na Pemba.

Alisema awali kulikuwa na changamoto ya mawasiliano kati ya Unguja na Pemba kutokana na kutumia teknolojia ya Mawimbi ya Radio, kupitia Mkongo wa Zanzibar na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano visiwa vya Unguja na Pemba vitakuwa vimeunganishwa kwenye miundombinu ya mawasiliano.

Chanzo: habarileo.co.tz