Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TTB kuweka mikakati ya kutangaza utalii

Utalii Mwenyej.jpeg TTB kuweka mikakati ya kutangaza utalii

Tue, 27 Jun 2023 Chanzo: Habarileo

BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imesema ipo kwenye utekelezaji wa mikakati miwili ya utangazaji utalii wa Kusini mwa Tanzania kuanzia mwaka 2021-2026. Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Damasi Mfugale alisema mikakati hiyo imetaja njia za utangazaji wa utalii ikiwa ni pamoja na kutumia watu maarufu/mabalozi wa hiari, utangazaji kwa njia ya mtandao, vyombo vya habari, ziara za mafunzo na kushiriki katika maonesho ya kibiashara.

Mfugale alisema hayo Dar es Salaam wakati wa kuhitimisha ziara ya utalii Kusini mwa Tanzania iliyofanywa na Balozi wa Hiari, Nicholas Reynolds maarufu kama Bongozozo kuunga mkono filamu ya: ‘Tanzania The Royal Tour’.

Ziara hiyo ilifanyika kuanzia Juni 12 hadi 24, 2023 katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania kwa kutembelea vivutio sita. Vivutio vilivyotembelewa ni pamoja na Hifadhi za Taifa za milima Udzungwa, Ruaha na Nyerere, pori la akiba la Mpanga Kipengere, kikundi cha utalii wa kitamaduni–Mtera Izazi na hifadhi ya urithi wa utamaduni wa dunia magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.

Mfugale alisema lengo la ziara hiyo ni kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana Kusini mwa Tanzania ili kuongeza ufahamu na kuongeza idadi ya watalii.

“Pia kuleta ushawishi kwa Watanzania kutembelea vivutio hivyo ambapo TTB ilifanya ubia na makampuni kutoka Kusini ambazo waliweza kuuza vifurushi na kuleta watalii ili kutalii na Bongozozo ikiwemo na vifurushi hivyo vilileta Watanzania 63 na Muingereza mmoja waliotembelea milima Udzungwa, Ruaha na Nyerere na pori la akiba la Mpanga Kipengere,”alieleza Mfugale.

Aliongeza: “Katika utekelezaji huo, TTB iliwasiliana na Bongozozo toka mwaka 2019 kwa wazo la safari ya mafunzo Kusini mwa Tanzania Juni, 2023 kwa jumla ya siku 13 ili kuunga mkono Rais Samia Suluhu katika jitihada zake za kutangaza Tanzania kupitia Filamu ya Royal Tour.”

Bongozozo alisema amefurahishwa sana na utalii wa Kusini kwani ameweza kujionea na kufurahia vivutio mbalimbali. Alisema katika ziara hiyo wamerekodi video katika maeneo mbalimbali ili kusambaza katika akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Chanzo: Habarileo