Usafiri kuelekea mikoa ya kaskazini huenda ukaimarika zaidi katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka kufuatia kuboreshwa kwa miundombinu ikiwemo kuongezwa kwa idadi ya mabehewa.
Tayari Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanza kufanya majaribio ya mabehewa mapya 22 yaliyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya reli ya kati na kaskazini.
Taarifa iliyotolewa leo Jumapili Desemba 11, 2022 na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiani wa shirika hilo, Jamila Mbarouk imesema majaribio ya mabehewa hayo yameanza kwa kuyasafirisha umbali wa kilomita 400 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro huku ukiwepo pia mpango wa kuyafanyia majaribio kutoka Dar hadi Kigoma.
“Hivi karibuni tunatarajia kuanza kutoa huduma ya usafiri wa reli kwa kutumia mabehewa haya mapya na kuongeza idadi ya safari katika reli ya kati na kaskazini ili kuwahudumia wananchi wanaotumia usafiri wa reli nchini,”amesema Jamila katika taarifa hiyo.
Kulingana na taarifa hiyo mabehewa hayo 22 yametengenezwa na kampuni ya Sung Shin Rolling Stock Technology ya Korea Kusini.
Kati ya mabehewa hayo, manne ya daraja la kulala, sita ta daraja la pili kukaa, 10 daraja la tatu kukaa na mabehewa mawili yaliyotengenezwa kutoa huduma za chakula kwa wasafiri.