Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TRC yaokoa bil 10/- za vichwa vya treni

Ccf019b2411a9f851a9b8e6fbac74676.jpeg TRC yaokoa bil 10/- za vichwa vya treni

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHIRIKA la Reli Tanzania(TRC) limeokoa zaidi ya Sh bilioni 10 baada ya kufufua vichwa saba vya treni na kuviongezea nguvu kutoka ‘horse power’ 760 hadi 800.

Vichwa hivyo vilivyonunuliwa mwaka 1979 awali vilikuwa na uwezo wa kuvuta tani 320 za mizigo lakini sasa vitavuta 400.

Mafundi wazalendo wengi wao wakiwa hawajapitia mifumo rasmi ya elimu ya ufundi wamefufua vichwa hivyo kwenye karakana kuu ya reli mkoani Morogoro.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilitembelea karakana hiyo mwishoni mwa wiki na kuitaka serikali iwape ajira za kudumu mafundi hao kwa kuwa ni hazina TRC.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Vichwa vya Treni TRC, Lameck Magandi aliieleza kamati hiyo kuwa karakana hiyo imekuwa ikifanya matengenezo madogo na makubwa.

Alisema mwaka 2013, serikali ilitoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa vichwa 16 vya treni vilivyonunuliwa mwaka 1979.

Magandi alisema vichwa hivyo vitaanza kufanya kazi muda wowote kuanzia sasa na ukarabati wa kichwa kimoja umegharimu Dola za Marekani 800,000.

Alisema changamoto kubwa inayoikabili karakana hiyo ni idadi kubwa ya mafundi ambao hawajaajiriwa kutokana na vigezo vya elimu.

Kamati ya Kudumu ya Bunge iliitaka serikali iweke utaratibu maalumu wa kuajiri mafundi waliopo kwenye karakana hivyo kwa kuwa wameonesha uwezo mkubwa.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa alisema karakana hiyo ilijengwa miaka ya 1970 na akatoa mwito kwa vyuo vifundishe vijana masuala ya reli.

Chanzo: www.habarileo.co.tz